Umoja wa Ulaya kutoa Euro bilioni 1.6 kwa Palestina
15 Aprili 2025Umoja wa Ulaya umetangaza mpango mpya wa msaada wa kifedha wa miaka mitatu kwa Wapalestina wenye thamani ya euro bilioni 1.6 .
Ahadi hiyo mpya ya msaada ilitolewa hapo siku ya Jumatatu wakati mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walipokutana na waziri mkuu wa Palestina Mohammed Mustafa huko Luxembourg katika mazungumzo ya kwanza yangazi ya juu, kati ya pande hizo mbili.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, amesema Umoja wa Ulaya unaongeza msaada kwa watu wa Palestina kusaidia kuleta utulivu katika Ukingo wa Magharibi na katika Ukanda wa Gaza.
Umoja wa Ulaya unatazamia kuiimarisha mamlaka ya Palestina wakati ambapo Israel imerejelea vita vyake huko Gaza baada ya kumalizika muda wa kusitishwa kwa mapigano.
Wakati huo huo amependekeza kuwekewa vikwazo zaidi, walowezi wa Israel "wenye msimamo mkali" katika Ukingo wa Magharibi, ingawa bado hakuna makubaliano kati ya nchi za moja wa Ulaya kuhusu hatua hiyo.