Umoja wa Ulaya kupitia upya makubaliano na Israel
21 Mei 2025Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisema baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja huo mjini Brussels kwamba sehemu kubwa ya mawaziri hao wameunga mkono pendekezo la kufanya upya mapitio ya kile kiitwacho "makubaliano ya ushirikiano" kutokana na yale yanayojiri kwenye Ukanda wa Gaza.
Mawaziri 17 kati ya 27 walilipitisha pendekezo hilo lililowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Uholanzi, Caspar Veldkamp, ambaye alitaka Umoja wa Ulaya ujielekeze kwenye kuhakikisha endapo Israel inaheshimu kifungu cha haki za binaadamu kilichomo kwenye makubaliano hayo.
Soma zaidi: Israel yakataa shinikizo la Umoja wa Ulaya kuhusu Gaza
"Hali ya Gaza ni majanga. Misaada iliyoruhusiwa kuingia na Israel ni hatua nzuri, lakini ni kama tone tu kwenye bahari. Misaada lazima iingie kwa wingi na kwa haraka, bila vikwazo, maana hicho ndicho kinachohitajika kwa sasa." Alisema Kallas.
Kauli kama hiyo imetolewa pia na Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka (MSF), ambalo limesema kwenye taarifa yake ya leo kuwa kiwango cha misaada kilichoruhusiwa kuingia Gaza na Israel hakitoshi hata kidogo na imekiita kuwa ni "kisingizio tu cha kuonesha ulimwengu kuwa mzingiro dhidi ya Ukanda huo umemalizika."
Kisingizio cha kukwepa lawama
Pascale Coissard, mratibu wa shirika hilo kwenye kitongoji cha Khan Younis, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba uamuzi wa mamlaka za Israel kuruhusu kiwango kidogo sana cha misaada kisichokwendana na hali kuingia Gaza baada ya miezi kadhaa ya mzingiro mkubwa, "unaashiria nia yao ya kukwepa tuhuma za kuwauwa watu kwa njaa, ilhali kiukweli ni kwamba wanaruhusu wapate chakula haba sana cha kuwafanya wavute pumzi tu."
Wakati Israel ikiwa imekabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa, ambalo haijawahi kulishuhudia tangu ianze vita vyake kwenye Ukanda huo, serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu imesema imefikia makubaliano na Israel kuruhusu kufikishwa kwa misaada muhimu ya kibinaadamu kwenye Ukanda wa Gaza.
Soma zaidi: Umoja wa Mataifa waruhusiwa kupeleka malori 100 ya misaada Gaza
Taarifa iliyotolewa na shirika rasmi la habari la Imarat, WAM, imesema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Falme hizo, Sheikh Abdullah bin Zayed, alizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Israel, Gideon Saar, ambapo hatimaye wamekubaliana kufikishwa kwa misaada hiyo, ambayo katika hatua ya awali itajumuisha chakula kwa raia 15,000 pamoja na mahitaji ya watoto wadogo.