Umoja wa Mataifa waunga mkono azimio kuhusu Ukraine
25 Februari 2025Hii ni mara ya kwanza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo ni chombo chenye nguvu zaidi cha Umoja wa Mataifa kufikia uamuzi wa pamoja juu ya vita.
Nchi kumi zilipiga kura ya kuunga mkono azimio hilo la Marekani, lakini mataifa matano yalijizuia.
Marekani, Urusi na China, zilipiga kura ya kuunga mkono, huku mataifa matano ya Ulaya kwenye Baraza hilo ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Slovenia, Denmark na Ugiriki yakijizuia. Kinadharia, Uingereza na Ufaransa zina haki ya kupinga azimio, lakini hawajaitumia mamlaka hiyo tangu 1989.
Waraka uliopitishwa, uliopewa kichwa "Njia ya Amani," hauitaji Moscow kama mchokozi ama mvamizi katika vita hivyo na wala hatoi wito kwa Urusi kujiondoa nchini Ukraine.
Mabalozi wapinga azimio kuhusu Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa
Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Barbara Woodward, alilipinga waziwazi azimio hilo akisema haiwezekani kuwepo na usawa kati ya Urusi na Ukraine, linapokuja suala la vita hivi na namna ambavyo Baraza hili inavitazama.
Kura hii imepigwa wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka mitatu ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine.
Soma pia:Umoja wa Ulaya yaadhimisha miaka mitatu ya vita vya Ukraine
Amesema "Wanajeshi wa Urusi wametumia ubakaji, mateso na mauaji kama silaha za vita na kuuweka hatarini usalama wa nyuklia. Hivi ni vita ambavyo Putin alisema vitachukua siku tatu, lakini miaka mitatu baadae, watu wa Ukraine bado wanaendelea kuumia."
Balozi wa Ufaransa Nicolas de Rivière alisema haiwezekani kuwepo amani na usalama ikiwa uonevu utapewa nafasi.
Balozi wa Marekani Dorothy Shea alipozungumzia azimio hilo alisema ni hatua ya kwanza inayofungua njia kuelekea kupatikana amani. Amesisitiza ni hatua ya kwanza, lakini muhimu mno ambayo wanapaswa kujivunia. Ametoa wito wa azimio hilo kutumika kama msingi wa mustakabali wa amani sio tu nchini Ukraine, bali pia Urusi na jamii ya kimataifa.
Soma pia:China yaunga mkono mpango wa Marekani wa amani Ukraine
Mapema, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha azimio sambamba na mataifa ya Ulaya, lakini Marekani ilijitenga nalo. Azimio hilo liliitaja Urusi kama mchokozi kwenye vita hivyo na kuitaka kuyaondoa majeshi kwenye eneo la Ukraine.
Urusi iliivamia Ukraine kikamilifu Februari 24, 2022. Gharama za kuujenga upya uchumi wa taifa hilo ulioathiriwa na uvamizi huo, imeongezeka na kufikia dola bilioni 524, hii ikiwa ni kulingana na utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya na serikali ya Ukraine.