UN yaikosoa Ujerumani kuwarejesha wakimbizi Afghanistan
4 Julai 2025Matangazo
Kauli ya UNHCR imetolewa baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt, kusema kwamba, anatarajia kuzungumza na utawala wa Taliban ili kuiwezesha Ujerumani kuwarejesha nyumbani raia hao wa Afghanistan.
Mwakilishi wa shirika hilo Arafat Jamal akizungumzia mpango huo amesema wanayatolea wito mataifa kutowarejesha nyumbani Waafghanstan kwa nguvu kwa kuwa hali nchini humo bado haijatengamaa.
Kwa upande wake msemaji wa ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani ameukataa pia mpango huo akisema bado kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu chini ya utawala wa Taliban.