UM: Ni lazima misaada iongezwe kusaidia nchi masikini
1 Julai 2025Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliufungua mkutano huo jana Jumatatu huku akiuhimiza ulimwengu "kufufua injini ya maendeleo" katikati ya kitisho kinacholetwa na hatua ya Marekani ya kupunguza misaada na ambacho kinaweza kuwa na athari kubwa katika vita dhidi ya umaskini na vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Guterres aidha alisema theluthi mbili ya malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa yaliyowekwa kwa mwaka 2030 yalikuwa "yamechelewa" na zaidi ya dola trilioni 4 za uwekezaji wa kila mwaka zinahitajika ili kufikia malengo hayo.
Rais Donald Trump wa Marekani amesitisha misaada kupitia shirika la Maendeleo la USAID, huku mataifa mengine tajiri kama Ujerumani, Uingereza na Ufaransa pia yakipunguza ufadhili na kuongeza fedha kwenye bajeti zao za ulinzi. Shirika la misaada la Oxfam limesema punguzo hili la ufadhili ni kubwa kabisa tangu 1960. Kulingana na Benki ya Dunia kuongezeka kwa umaskini uliokithiri kunaathiri zaidi mataifa yaliyoko Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kulingana na Guterres, masuala kuanzia ya ushuru wa Trump hadi mivutano huko Mashariki ya Kati na Ukraine kwa pamoja yanatatiza biashara ya kimataifa na kuathiri kubwa mshikamano wa kidiplomasia unaohitajika katika juhudi za kuzisaidia nchi kuondokana na umaskini.
Viongozi wa dunia na zaidi ya wawakilishi 4,000 kuanzia wafanyabiashara, mashirika ya kiraia hadi taasisi za fedha wako katika mji wa Seville kwenye mkutano huo unaolenga kusaka msukumo mpya wa ufadhili wa maendeleo.
Lengo kuu ni kusaidia mataifa masikini kuinuka
Miongoni mwa masuala muhimu kwenye kusanyiko hilo ni mageuzi katika masuala ya fedha ya kimataifa ili kuzisaidia nchi maskini zaidi kuutua mzigo wa madeni unaozidi kurudisha nyuma maendeleo. Deni la nje la nchi masikini zaidi limeongezeka zaidi ya mara tatu katika kipindi cha miaka 15, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Rais wa Kenya William Ruto alisema bado kuna ulazima wa ufadhili wa kimataifa, na kwamba Afrika haiombi kupewa upendeleo, bali wanachotaka ni usawa, ushirikiano na uwekezaji, huku akiiomba Marekani kufikiria upya msimamo wake.
Kwenye mkutano huo aidha kulitolewa tamko la pamoja lililothibitisha mataifa yatakavyojitoa katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa kama vile kuondoa umaskini na njaa, kukuza usawa wa kijinsia, kurekebisha mifumo ya kodi na taasisi za fedha za kimataifa.
Waraka huo pia umetoa wito kwa benki za maendeleo kuongeza uwezo wao wa kukopesha mara tatu, kuwataka wakopeshaji kuhakikisha kunakuwepo fedha kwa ajili ya matumizi muhimu ya kijamii lakini pia kuimarisha mapambano dhidi ya ukwepaji kodi.
Katika hatua nyingine, nchi zikiwemo Ufaransa, Kenya, Barbados na Uhispania hapo jana zilizindua muungano wa kushinikiza ushuru kwa matajiri wanaotumia usafiri wa anga ili kusaidia mataifa maskini kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, ofisi ya rais wa Ufaransa imesema.
Muungano huo, ambao pia unazileta pamoja Somalia, Benin, Sierra Leone na Antigua na Barbuda, ulisema utahakikisha unaongeza idadi ya nchi zinazotoza ushuru tikiti za ndege, zikiwemo za usafiri wa daraja la kibiashara, na ndege za binafsi.
Sekta ya anga ni chanzo kikuu cha uchafuzi wa hewa na kuchangia ongezeko la joto duniani, linaloleta athari mbaya zaidi kwa nchi zinazoendelea.