Umoja wa Mataifa wataka mauaji ya raia yakomeshwe Syria
9 Machi 2025Kamishna Mkuu wa haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, ameitolea wito serikali ya mpito ya Syria kuzuia mauaji ya raia katika eneo hilo na kutaka mapigano haraka mara moja.
Wakati huo huo, mapigano yameripotiwa Jumapili katika mtambo wa gesi wa Banias nchini Syria. Kulingana na shirika la habari la SANA, mapambano hayo yameibuka baada ya kutokea kwa shambulio lililofanywa na wafuasi waliosalia wa utawala wa serikali iliyoangushwa ya Bashar al-Assad.
Soma zaidi: Ahmed al-Sharaa atoa wito wa kudumisha amani Syria wakati machafuko yakiendelea
Kamanda wa vikosi vya Syrian Democratic- SDF, vinavyoongozwa na Wakurdi Mazloum Abdi amesema Rais wa mpito wa nchi hiyo Ahmed al-Sharaa anapaswa kuwawajibisha wahusika wa machafuko yaliyoibuka katika maeneo ya Pwani ya nchi hiyo.
Nayo Ujerumani imesema ripoti za kuuwawa kwa watu 1,000 katika Pwani ya Syria kwenye machafuko ya hivi karibuni ni za kushtusha. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema serikali ya mpito ya Syria ina wajibu wa kuzuia mashambulio mengine, kuchunguza matukio na kuwawajibisha waliohusika.