UN yatahadharisha kuhusu vita vya kikanda
17 Februari 2025Antonio Guterres ameitoa kauli hiyo siku ya Jumamosi alipohudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika uliofunguliwa mjini Addis Ababa, Ethiopia huku akitoa pia wito wa kuheshimu mipaka ya Kongo:
"Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, raia wa Kongo wanateseka kutokana na mzunguuko wa ghasia za kikatili. Na mapigano yanayoendelea huko Kivu Kusini kufuatia kusonga mbele kwa M23, yanatishia kulitumbukiza eneo lote kwenye janga. Ni lazima kuepusha kwa gharama yeyote, kuongezeka kwa mizozo ya kikanda. Hakuna suluhisho la kijeshi. Hali lazima isitishwe na mazungumzo yaanzishwe tena. Na uhuru na mipaka ya DRC ni lazima viheshimiwe."
Huku Rwanda ikikabiliwa na shinikizo la kimataifa ili kusitisha mapigano mashariki mwa Kongo , mzozo huo umegubika mazungumzo katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.
Rais wa Rwanda Paul Kagame alihudhuria mkutano huo, lakini rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi hakuwepo licha ya M23 kupata mafanikio makubwa katika uwanja wa mapambano kwa kuchukuia udhibiti wa miji mikuu ya mashariki mwa Kongo ya Goma na Bukavu.
Mizozo yagubika mijadala katika mkutano wa kilele wa AU
Viongozi wa mataifa ya Afrika wamekutana mjini Addis Ababa Jumamosi kwa mkutano wa kilele wa siku mbili wa Umoja wa Afrika unaofanyika chini ya kiwingu cha mzozo wa mashariki mwa Kongo na vita nchini Sudan.
Mkutano huo umefunguliwa wakati juhudi za kidiplomasia zimeshindwa kuutatua mzozo wa Kongo ambapo waasi wa M23 wanaendelea kusonga mbele na jana wameukamata mji mwingine mkubwa wa Bukavu mashariki mwa nchi hiyo.
Huku hali ya taharuki ikishuhudiwa ikiongezeka katika kanda zima kutokana na mzozo huo wa mashariki mwa DRC, Umoja wa Afrika umekuwa ukikosolewa kwa msimamo wake usio thabiti huku waangalizi wakiitaka AU kuchukua hatua zaidi na zilizo madhubuti.
Kwa upande mwingine, Umoja wa Ulaya umesema siku ya Jumamosi kuwa uko tayari kwa hatua zote za haraka kufuatia taarifa za kutekwa kwa mji wa Bukavu na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.
Soma pia: Tshisekedi kutohudhuria kikao cha AU juu ya vita vya DRC
Mbali ya mizozo, mkutano wa Umoja wa Afrika unatarajiwa kumchagua mwenyekiti mpya wa Halmashauri Kuu ya umoja huo atakayechukua nafasi ya Moussa Faki Mahamat anayemaliza muda wake. Wagombea watatu ikiwemo mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga wanawania nafasi hiyo.
Mwenyekiti wa tume ya AU anayemaliza muda wake Moussa Faki Mahamat ameliambia shirika la habari la AFP siku ya Ijumaa kwamba kulikuwa na "uhamasishaji wa jumla" miongoni mwa mataifa ya Afrika ili kusitisha mapigano huko DRC.
Mkuu wa jeshi la Uganda atishia kuushambulia mji wa Bunia
Mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba amesema katika chapisho lake katika mtandao wa kijamii wa X kwamba wanaweza kuushambulia mji wa Bunia uliopo mashariki mwa Kongo ikiwa vikosi vyote vilivyopo katika eneo hilo havitojisalimisha ndani ya masaa 24.
Kainerugaba, ambaye ana historia ya kuchapisha maoni yenye utata juu ya mambo mbalimbali amesema ana mamlaka aliyopewa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, ambaye pia ni baba yake. Lakini hata hivyo msemaji mkuu wa jeshi la Uganda amesema hawawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa.
Soma pia: Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika wafunguliwa mjini Addis Abbaba
Tishio hilo kutoka kwa afisa mkuu wa kijeshi wa Uganda, ambaye anatazamiwa kuwa mrithi wa baba yake linazidisha hofu kwamba mzozo kati ya vikosi vya Kongo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda unaweza kugeuka na kuwa vita vya kikanda.
Siku ya Ijumaa, waasi wa M23 waliingia kwenye mji wa pili kwa ukubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wa Bukavu.
(Vyanzo: AP, Reuters, AFP)