Umoja wa Mataifa waonya kuhusu dhulma dhidi ya Wapalestina
15 Julai 2025Umoja wa Mataifa umetahadharisha juu ya idadi kubwa kabisa ya Wapalestina wanaohamishwa kwa nguvu kutoka eneo la Ukingo wa Magharibi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1967, karibu miaka 60 iliyopita. Umoja wa Mataifa umesema operesheni ya jeshi la Israel iliyoanzishwa kaskazini mwa eneo hilo mnamo Januari wmaka huu imesababisha maalfu ya watu kuyahama makazi yao, na hivyo kuibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa mauaji ya safisha safisha ya kikabila.
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Umoja wa Mataifa linaoshughulikia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Juliette Touma, amesema operesheni hiyo imekuwa ndefu zaidi tangu intifada ya pili ya Wapalestina mwanzoni mwa miaka ya 2000, na inaziathiri kambi kadhaa za wakimbizi katika eneo hilo. Akizungumza na waandishi habari kwa njia ya video mjini Geneva akiwa nchini Jordan, Touma amerejelea vita va siku sita kati ya nchi za kiarabu na Israel vilivyosababisha Israel kuukalia Ukingo wa Magharibi.
Afisi ya haki ya Umoja wa Mataifa imetahadharisha kwamba kuwaondoa idadi kubwa ya watu kwa nguvu kunakofanywa na nchi inayolikalia eneo huenda kukawa ni safisafisha ya kikabila.
Msemaji wa afisi hiyo Thameen Al-Kheetan amesema tangu Israel ilipoanzisha operesheni yake iliyopeewa jina Iron Wall - Ukuta wa Chuma kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi mnamo Janauri 2025, Wapalestina kiasi 30,300 wamelazimishwa kuyahama makazi yao.
"Walowezi wa Israel na vikosi vya usalama wameimarisha na kuongeza mauaji, mashambilizi, udhalilishaji na mateso ya Wapalestina katika maeneo yanayokaliwa ya Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Jerusalem Mashariki, katika wiki chache zilizopita. Hii ni pamoja na uvunjaji wa mamia ya makazi na kuwalazimisha Wapalestina waondoke makwao, hali inayosaidia kufanikisha kutekwa na kuchukuliwa kwa eneo la Ukingo wa Magharibi na Israel kinyume cha sheria ya kimataifa."
Al-Kheetan aliongeza kusema, "Tangu kuazishwa kwa operesheni ya "Ukuta wa Chuma" kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi mapema mwaka huu, Wapalestina takriban 30,300 wamelazimishwa kuyahama makazi yao."
Afisi ya haki ya Umoja wa Mataifa pia imesema imerekodi mauaji kiasi 875 katika kipindi cha wiki sita zilizopita katika vituo vya misaada katika Ukanda wa Gaza vinavyoendeshwa na wakfuw a misaada wa Gaza unaoungwa mkono na Marekani na Israel, na misafa inayosimamiwa na mashirika mengine ya misaada, ikiwemo Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa afisi hiyo Thameen Al-Kheetan amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba watu 674 waliuliwa karibu na vituo vya wakfu huo na wengine 201 wakauwawa katika njia za misafara mingine ya misaada.
Umoja wa Ulaya wapanga kuichukulia hatua Israel kuhusu Gaza
Ripoti hii imetolewa wakati Umoja wa Ulaya uliogawika ukitafakari kuichukulia hatua Israel kuhusu vita vya Gaza. Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya leo wamejadili hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya Israel lakini hawakuonesha dalili ya kukubaliana na hatua yoyote angalau moja.
Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Kaja Kallas aliwasilisha hatua kumi baada ya Israel kukiuka mkataba wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili kwa msingi wa haki za binadamu. Hatua hizo zinajumuisha kuusitisha mkataba wote au kudhibiti mashirikiano ya kibiashara mpaka kuwawekea vikwazo mawaziri wa Israel, kikwazo cha silaha na kusitisha safari bila visa.
Israel yashambulia maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon
Wakati haya yakiarifiwa, jeshi la Israel IDF limesema limezishambulia ngome za kundi la Hezbollah nchini Lebanon. Ndege za kivita zimeyalenga maeneo ya kijeshi katika bonde la mashariki la Bekaa, ambalo Hezbollah hulitumia kwa mafunzo. Maeneo hayo yanamilikiwa na kikosi maalumu cha Hezbollah cha Radwan. Wizara ya afya ya Lebanon imesema watu wapatao sita wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo.
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema mashambulizi ya nchini Lebano yanatuma ujumbe wa wazi kwa Hezbollah, akilituhumu kundi hilo la wanamgambo wa kiislamu linaloungwa mkono na Iran kwa kujaribu kuvijenga upya vikosi vyake kinyume na mkataba wa usitishaji mapigano ulioafikiwa.
Israel yashambulia kusini mwa Syria
Wakati huo huo, Israel imefanya mashambulizi kusini mwa Syria katika kile inachosema ni hatua ya kuilinda jamii ya Druze kufuatia kuepelekwa kwa vikosi vya serikali ya Syria katika mji wenye idadi kubwa ya wakazi wa jamii hiyo wa Sweida.
Katika taarifa ya pamoja, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa ulinzi Israel Katz, wamesema hatua hiyo imechukuliwa kuuzuia uongozi wa Syria kuwadhuru au kuwaumiza watu wa jamii ya Druze na kuhakikisha hakuna silaha wala shughuli zozote za kijeshi katika eneo hilo linalopatikana karibu na mpaka wa Israel.
Netanyahu na Katz wameueleza uwepo wa vikosi vya Syria na silaha kama kitisho cha usalama.