Umoja wa Mataifa waonya athari za joto kali kwa wafanyakazi
22 Agosti 2025Ripoti iliyotolewa kwa pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa la Umoja wa Mataifa (WMO) inasema wafanyakazi bilioni 2.4 ulimwenguni, ambao ni sawa na asilimia 71 ya wafanyakazi wote, wamekuwa wakifanya kazi zao wakiwa kwenye mazingira ya joto kali sana.
Mkurugenzi wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Uhamaji wa WHO, Rüdiger Krech, alisema miongoni mwa madhara ya moja kwa moja yanayowapata wafanyakazi hao ni maradhi ya kiharusi, figo, miili kukauka maji, na magonjwa mengine makubwa zaidi.
"Kwenye sekta za kilimo, ujenzi na kazi nyengine zinazohitaji wafanyakazi wa nguvu kazi, tunashuhudia ongezeko kubwa la maradhi ya kiharusi yanayotokana na joto kali, madhara ya muda mrefu kwa figo na mishipa ya fahamu kutokana na mazingira mabaya ya kazi." Alisema mkurugenzi huyo akiongeza kwamba wafanyakazi, ambao ndio wanaozifanya jamii zistawi wanalipia gharama kubwa sana.
"Athari hizi ni mbaya zaidi kwenye jamii ambazo hazina vifaa vya kupoza hewa, huduma za afya na sera za kuwalinda wafanyakazi." Alisema Krech.
Wafanyakazi 19,000 wapoteza maisha kila mwaka
Shirika la Kazi Duniani (ILO) linakisia kuwa madhara yatokanayo na mazingira ya kazi yanasababisha wafanyakazi 19,000 kupoteza maisha kila mwaka huku wengine milioni 22 wakijeruhiwa, baadhi katika kiwango ambacho hawawezi tena kufanya kazi.
Mkuu wa Kitengo cha Usalama, Afya na Mazingira ya Kazi wa ILO, Joaquim Pintado Nunes, aliwaambia waandishi wa habari kuwa endapo hatua hazikuchukuliwa haraka iwezekanavyo, kuna hatari za kulipoteza tabaka muhimu la wafanyakazi kwenye maafa na maradhi yanayoweza kuepukika.
"Mabadiliko ya tabianchi yanaiunda upya dunia ya wafanyakazi, na tunachoweza kusema ni kwamba bila hatua kali zilizoratibiwa vyema, basi mfadhaiko unaotokana na joto kali utakuwa mojawapo ya majanga makubwa kabisa kazini katika zama zetu, utasababisha kupotea kwa maisha ya watu wengi, kupotea kwa uzalishaji mwingi, na matokeo mabaya kabisa kwenye mustakabali wa kazi duniani." Alisema Nunes, akiongeza kwamba dunia haiwezi tena kusubiri na "lazima sauti za pamoja za serikali, waajiri na wafanyakazi zisikike."
Ripoti hii mpya iliyoambatana na muongozo wa kiufundi inaonya kwambamabadiliko ya tabia nchi yamesababisha fukuto la joto kuzidi kusambaa na kusababisha hasara kubwa kwenye afya na utendaji wa wafanyakazi, hasa miongoni mwa wafanyakazi wa vibarua kwenye kilimo, ujenzi na uvuvi, na makundi mengine ya wale wenye vipato vya chini.
Yakitumia uzoefu wao wa miongo mitano ya utafiti na kukusanya ushahidi, mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yametowa muongozo wa wazi kwa serikali, waajiri na mamlaka za afya kuutumia ili kukabiliana na ongezeko kubwa la joto kwenye maeneo yenye kiwango kikubwa cha wafanyakazi.