UN yamtaka Trump kutengua amri ya vikwazo dhidi ya ICC
7 Februari 2025Baada ya Donald Trump kusaini agizo la kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC, Umoja wa Mataifa umemtaka kiongozi huyo kuubadilisha uamuzi wake ukisema mahakama hiyo ni sehemu muhimu ya kutetea haki za binadamu duniani.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema inaunga mkono kikamilifu kazi huru ya chombo hicho katika hali zote kinapotimiza majukumu ndani ya mamlaka yake.
Soma zaidi: Marekani yaiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC
Mapema Alhamisi, Donald Trump alitia sahihi agizo la kuzishikilia mali la maafisa, waajiriwa na ndugu wa wafanyakazi wa mahakama hiyo pamoja na kuwapiga marufuku kuingia Marekani. Anaishutumu ICC kwa matumizi mabaya ya madaraka na kwa kutoa waranti wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant.
Naye Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema mahakama ya ICC inapaswa kuwa na uwezo wa kufanya shughuli zake kwa uhuru katika mapambano dhidi ya wahalifu wanaokwepa mkono wa sheria kote duniani bila vizuizi.
Mataifa mengine ya Ulaya yakosoa ICC kuwekewa vikwazo
Aidha, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pia amekosoa hatua ya chombo hicho cha kimataifa cha sheria kuwekewa vikwazo. Amesema kuwa, ''Sidhani kama ni sahihi kuiwekea vikwazo mahakama ya ICC. Bila shaka ni sahihi kabisa kukasirika kuhusu baadhi ya masuala, kupishana kauli na kusimama mahakamani ukiwa na misimamo yako. Lakini kuiwekea vikwazo si jambo sahihi. Wanahatarisha taasisi inayopaswa kuhakikisha kuwa madikteta wa dunia hii hawawatesi watu na kuanzisha vita. Na hilo ni muhimu.''
Akizungumzia suala hilo hilo, msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Stammer amesema nchi yake inaunga mkono uhuru wa ICC na haina mpango wa kuwawekea vikwazo maafisa wake. Ufaransa yenyewe, imesisitiza kuwa itaendelea kuiunga mkono ICC na kuwahamasisha washirika wake ili mahakama hiyo iendelee na kazi zake kwa uhuru.
Ukraine nayo kupitia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje Heorhii Tykhyi imesema inaamini kuwa kazi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita hasa katika kuhakikisha wahalifu wa kivita wa Urusi wanawajibishwa.
Katika hatua nyingine, mwanasheria anayewawakilisha takriban waathiriwa 350 wa shambulio lililofanywa na kundi la Hamas nchini Israel Oktoba 7 Yael Vias Gvirsman, amesema wataendelea kufanya kazi na ICC hata baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuiwekea vikwazo.