UN yahimiza usuluhishi wa amani wa migogoro
23 Julai 2025Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limezihimiza nchi 193 wanachama wa umoja huo zitumie njia zote zinazowezekana kusuluhisha migogoro kwa amani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema muelekeo huo unahitajika sana kwa sasa kuliko wakati mwingine, alipotaja hali ya kutisha katika Ukanda wa Gaza na mizozo inayoendelea nchini Ukraine, Sudan, Haiti na Myanmar.
Akihimiza juhudi zaidi zifanyike kutafuta amani ya dunia, Guterres ameliambia baraza la usalama kwamba kote duniani kunashuhudiwa hali ya kutoheshimu wala kuzingatia sheria ya kimataifa pamoja na mkataba wa Umoja wa Mataifa.
" Kushindwa huku kutimiza wajibu wa kimataifa kunakuja wakati kukishuhudiwa migawanyiko na migogoro ya kilimwengu inayoongezeka. Na gharama yake ni kubwa hasa kwa maisha ya binaadamu, kusambaratisha jamii na kuharibu mustakabali wetu."
Guterres amesema huenda diplomasia haikufanikiwa kila mara kusuluhisha migogoro, machafuko na kukosekana uthabiti, lakini ina nguvu kubwa ya kuizuia.