Umoja wa Mataifa una wasiwasi kuhusu njaa Gaza
28 Agosti 2025Katika mkutano wa Jumatano, wanachama wa baraza hilo wameonya kwamba kutumia njaa kama silaha ya kivita ni kinyume na sheria za kimataifa za kiutu.
Wameelezea tahadhari na masikitiko yao makubwa kufuatia ripoti ya njaa iliyotolewa na Shirika la Kutathmini Usalama wa Upatikanaji wa Chakula Duniani, IPC, Ijumaa iliyopita.
Wamesema kuwa wanaiamini ripoti hiyo ambayo imethibitisha kwa mara ya kwanza kwamba njaa imelikumba eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura na Kiutu ya Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya amesema zaidi ya watu nusu milioni Gaza wanakabiliwa na njaa kwa sasa, umaskini na kifo.
Kulinga na Msuya, idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia watu 640,000 ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba. Amesema hakuna mtu ambaye hajaguswa na njaa katika Ukanda wa Gaza.
Israel imetaka kuondolewa mara moja kwa ripoti ya IPC, ikisema kuwa ni ya ''kutengenezwa,'' iliyochochewa kisiasa.
Wakati huo huo, shirika la ulinzi wa kiraia la Gaza, limesema kuwa takribani Wapalestina 39 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel siku ya Jumatano katika Ukanda wa Gaza.