UN na Brazil kufanya mkutano kuelekea COP30
23 Aprili 2025Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva atafanya mkutano kupitia mtandao na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatano kujadili kuimarisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa kabla kufanyika mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa COP30.
Msemaji wa Guterres, Stephane Dujarric amesema katibu mkuu huyo na rais Lula watafanya kikao kidogo cha faragha kitakachowashirikisha wakuu wa dola na serikali kujadili njia za kuimarisha juhudi za ulimwengu katika kukabiliana na mgogoro wa hali ya hewa na kuharakisha kipindi cha mpito kuelekea matumizi ya nishati safi isiyochafua mazingira.
Dujarric aidha amesema lengo la mkutano huo ni kuimarisha mdahalo kuhusu mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa kabla mkutano wa COP30 uliopangwa kufanyika katika mji wa Belem eneo la Amazon baadaye mwaka huu utakaoadhimisha muongo mmoja tangu kusainiwa mkataba wa Paris.