Ghasia zaongezeka dhidi ya Wapalestina Ukingo wa Magharibi
15 Julai 2025Msemaji wa Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Thameen Al-Kheetan, amewaambia waandishi habari siku ya Jumanne mjini Geneva kwamba mashambulizi hayo yanafanywa na walowezi na vikosi vya usalama katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu katika wiki za hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Al-Kheetan tangu mwezi Januari, kumekuwepo na mashambulizi 757 yaliyofanywa na walowezi dhidi ya Wapalestina au mali zao.
Idadi hiyo ni nyongeza ya asilimia 13 katika kipindi sawa na hicho mwaka uliopita.
Al-Kheetan amesema Wapalestina 96 walijeruhiwa mwezi Juni pekee, hiyo ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya kila mwezi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyopita.
''Israel lazima ikomeseha mara moja mauaji haya, unyanyasji na kuvunja nyumba katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kimabavu. Israel inapaswa kuchukua hatua zinazowezekana ili kuhakikisha kuna utulivu na usalama wa umma kwenye Ukingo wa Magharibi,'' alisisitiza Al-Kheetan.
Takribani Wapalestina 964 wameuawa na wanajeshi wa Israel pamoja na walowezi tangu Oktoba 7, mwaka 2023, katika Ukingo wa Mgharibi, ikiwemo Jerusalem Mashariki.