AU yasema haiitambui serikali mbadala ya Sudan
30 Julai 2025Umoja wa Afrika kupitia Baraza lake la Amani na Usalama umetangaza kutoutambua utawala uliotangazwa na kundi la Rapid Support Forces, RSF, na washirika wake, katika maeneo wanayoyadhibiti magharibi na kusini mwa Sudan. Umoja huo umezitaka nchi wanachama na jumuiya ya kimataifa kutounga mkono kile kilichoitwa ''serikali nyingine iliyotangazwa na RSF,'' ikisema inauweka rehani mustakabali wa taifa hilo.
Tangazo la RSF la kuunda serikali mbadala lilitolewa tarehe 27 Julai, na kupokelewa kwa upinzani si tu kutoka kwa Umoja wa Afrika, bali pia Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, na Saudi Arabia. Wote wametoa msimamo wa kuitambua tu serikali ya kiraia iliyoanzishwa mjini Port Sudan, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Kamil Idris.
Mapigano makali kati ya jeshi na RSF yaripotiwa El-Fasher
Mjumbe wa Umoja wa Afrika nchini Sudan, Mohammed Belaiche, amepongeza kuundwa kwa serikali hiyo ya kiraia akisema ni hatua muhimu kuelekea kupunguza mateso ya wananchi, kuboresha huduma, na kuruhusu wakimbizi kurejea nyumbani. Pia alisifu juhudi za jeshi la Sudan katika kulinda utulivu na kupambana na kile alichokiita "uasi".
Katika ulingo wa kimataifa, juhudi za mazungumzo pia zimegubikwa na migawanyiko. Mkutano uliopangwa kufanyika mjini Washington kati ya Marekani, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE na Misri ulishindikana kutokana na kutokubaliana kuhusu nafasi ya jeshi na RSF katika kipindi cha mpito wa kisiasa. UAE ilitaka pande zote mbili ziondolewe kwenye mchakato huo, lakini Misri ikasisitiza kulindwa kwa taasisi za taifa kama jeshi.
Mashirika ya misaada: Sudan yakabiliwa na mzozo mkubwa wa kibinaadamu
Wakati siasa zikiwa bado zimetatizika, baadhi ya wakimbizi waliokuwa wamekimbilia nchi jirani, hasa Misri, sasa wameanza kurejea nyumbani kwa hiari. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM, zaidi ya watu 190,000 wamevuka mpaka kutoka Misri kuingia Sudan tangu mwanzo wa mwaka huu.
Malaz Atef ni mmoja wa waliokuwa wakimbizi nchini Misri. Anasema amekuwa akisubiri kwa muda mrefu siku ya kurejea kwenye ardhi ya nyumbani.
"Kwa kweli, nina furaha sana kwamba tunarejea Sudan baada ya muda mrefu. Tuliikosa ardhi ya Nile, nyumbani, vikao vya familia na marafiki. Naikumbuka kila kona ya Sudan, kwa kweli. Nina furaha sana kurudi baada ya muda mrefu."
Mashirika ya misaada yaonya kuhusu mashambulizi dhidi ya hospitali Sudan
Safari za kurejea zinaanzia stesheni ya treni mjini Cairo, ambako familia nyingi zimekuwa zikisubiri treni za bure kuelekea Aswan, kabla ya kuendelea na mabasi hadi Khartoum. Ni safari ya matumaini, licha ya hofu ya hali ya usalama isiyoeleweka wazi.
Wakimbizi hawa wanarejea huku matumaini ya amani yakizidi licha ya mashaka ya vita. Na kwa wengi, kurejea nyumbani si tu hatua ya kijiografia, bali ni ahadi ya kuanza upya maisha yao waliyoachwa nayo katikati ya migogoro.