Umoja wa Afrika watoa wito wa usitishaji mapigano Libya
24 Mei 2025Umoja wa Afrika umetoa wito wa usitishaji kamili wa mapigano nchini LIbya. Haya ni kufuatia mapigano ya hivi karibuni katika mji mkuu Tripoli, na maandamano ya kudai kujiuzulu kwa waziri mkuu.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limekemea vikali ghasia hizo za mwanzoni mwa mwezi huu, na kutoa wito wa "kusitishwa mapigano bila masharti". Baraza hilo limehimiza pia "upatanisho wa kina unaoongozwa na Walibya wenyewe", na kuongeza kuwa "linatoa wito wa kutokuwepo kwa uingiliaji wa nje".
Mapigano ya hivi karibuni katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, inayokumbwa na mizozo, yaliwahusisha wapiganaji wa kundi la wanamgambo linaloiunga mkono serikali ya Tripoli dhidi ya makundi ambayo serikali hiyo imekuwa ikijaribu kuyasambaratisha, na kusababisha vifo vya takribani watu wanane, kulingana na Umoja wa Mataifa.