UM: M23 iliwaua watu 319 nchini Kongo mwezi Julai
7 Agosti 2025Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amelikosoa kwa matamshi makali kundi la waasi wa M23 linaloungwa mkono na Rwanda kwa mauaji ya takriban watu 319 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Julai.
Machafuko ya mwezi uliopita yametokea wiki chache baada ya serikali ya Kongo na M23 kutia saini tamko la pamoja mnamo Juni 19 mjini Doha, Qatar na kuthibitisha dhamira yao ya kusitisha mapigano ya kudumu.
Ofisi hiyo ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema imerekodi mashambulio mengi katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri, na kwamba ipo haja ya kukomeshwa mashambulizi yote dhidi ya raia na kuwajibishwa kwa waliohusika.
Hata hivyo, licha ya kusainiwa kwa mikataba mingi ya usitishaji mapigano na mapatano bado nchi hiyo imeshuhudia kuvunjwa kwa makubaliano hayo na kushindwa kumaliza mizozo ndani iliyodumu kwa zaidi ya miaka 30.