UM, AU zasifu mkataba wa amani Kongo na Rwanda
29 Juni 2025Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameutaja mkataba huo kuwa "hatua muhimu" kuelekea kupunguza uhasama baina ya mataifa hayo mawili jirani.
Pia ameipongeza Marekani kwa jukumu la upatanishi ilochukua na kufanikisha kupatikana mkataba huo.
Matamshi hayo ameyatoa baada ya Kongo na Rwanda kutia saini mkataba wa amani mjini Washington siku ya Ijumaa. Mkataba huo unalenga kumaliza miongo kadhaa ya mapigano mashariki mwa Kongo.
Guterres amezirai pande zinazohusika kutimiza kikamilifu ahadi walizotoa kwenye mchakato wa kutafuta amani na kile walichokubaliana na kukiidhinisha kupitia mkataba huo.
Amesema Umoja wa Mataifa umedhamiria kuunga mkono utekelezaji wa makubaliano hayo kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda na wadau wengine wa kimataifa.
Umoja wa Afrika: Ni "mafanikio makubwa" kuelekea amani
Kwa upande wake Umoja wa Afrika umesema mkataba huo wa amani ni "mafanikio makubwa" kuelekea kuleta amani kwenye moja ya maeneo tete zaidi duniani.
Kwa zaidi ya miaka 30 eneo la mashariki mwa Kongo limeshuhudia ghasia na machafuko, ambayo yamezidi makali mnamo miaka ya karibuni hasa kutokana na kuimarika kwa kundi la waasi linaloungwa mkono na Rwanda la M23.
Taarifa ya umoja huo imesema Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, aliyeshuhudia utiaji saini mkataba wa amani mjini Washington, "ameyakaribisha mafanikio hayo na kusifu jitihada zote zinazolenga kuleta amani, utulivu na maridhiano kwenye kanda hiyo".
Pia imesema Youssouf "anathamini mchango mkubwa uliotolewa na Marekani pamoja na Qatar katika kufanikisha mazungumzo yaliyowezesha kupatika mafanikio ya sasa".
Mkataba wapatikana baada ya jumuiya za kikanda kushindwa
Mkataba huo umepatikana baada ya kundi la M23 kusonga mbele kwa kasi mapema mwaka huu,ikayatwaa maeneo makubwa ya mashariki mwa Kongo ikiwemo miji muhimu ya Goma na Bukavu.
Rwanda imekuwa ikikataa madai ya kuliunga mkono kundi la M23 linaloundwa kwa sehemu kubwa na jamii ya Watutsi.
Serikali ya Kigali badala yake inaituhumu Kongo kuliunga mkono kundi la waasi la FDLR inalosema linatishia usalama wa Rwanda.
Inataka kutokomezwa kwa kundi hilo linaloundwa na jamii ya Wahutu waliohusika na mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi mwaka 1994.
Kufuatia hali hiyo, juhudi za upatanishi zilianza zikiongozwa kwanza na jumuiya za kikanda za Afrika Mashariki na ile ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, kisha baadae Umoja wa Afrika lakini hakuna mafanikio yaliyopatikana.
Qatar na baadae Marekani zikajipa jukumu la upatanishi na kufanikisha kupatikana mkataba wa amani.
Makampuni ya Marekani kunufaika na rasilimali za Kongo?
Hata hivyo mkataba huo hauelezi kinagaubaga mafanikio yaliyopatikana na M23 kwenye eneo la mashariki mwa Kongo na badala limeitolea mwito Rwanda kusitisha hatua zake zinazotajwa kuwa za "kujihami" ambazo imezichukua.
Mkataba uliopatikana umetoa mwito wa "kusambaratishwa" kwa kundi la FDLR.
Mkataba huo pia unagusia suala la kuheshimiwa kwa hadhi ya mipaka ya kila upande, kukomeshwa uhasama na kuvunjwa kwa makundi yote yenye silaha na kisha kujumuishwa ndani ya serikali.
Pia unalenga kufanikisha kurejea kwa wakimbizi wa ndani ya Kongo na kufanikisha kusambazwa misaada ya kiutu kwenye eneo lenye mzozo.
Yumkini Marekani itanufaika kwa kampuni za nchi hiyo kupewa kipaumbele katika kuvuna rasilimali hasa madini mashariki mwa Kongo.