Ulimwengu wakaribisha Usitishaji vita Iran na Israel
24 Juni 2025Mataifa mbali mbali ya Kiarabu na viongozi katika Jumuiya ya Kimataifa wamekaribisha hatua ya usitishaji vita kati ya Israel na Iran iliyotangazwa na rais wa Marekani Donald Trump usiku wa kuamkia leo.
Misri, Saudi Arabia na Jordan zimeipongeza hatua hiyo huku Misri ikisema itaendelea na juhudi zake za kidiplomasia na washirika kuudumisha usitishaji huo wa mapigano.
Hata hivyo waziri wa ulinzi waIsrael,Israel Katz amesema kwamba Iran imekiuka kabisa usitishaji huo wa vita kwa kufyetuwa makombora muda mfupi baada ya kuanza utekelezaji mpango huo. Iran imekanusha tuhuma hizo za Israel.
Sauti za miripuko na ving'ora vilisikika kwenye eneo zima la Kaskazini mwa Israel leo asubuhi baada ya nchi zote mbili kukubali mpango ya kusitisha vita vilivyodumu siku 12.
Waziri wa ulinzi wa Israel amesema ameliagiza jeshi kuanza upya mashambulio dhidi ya majengo ya jeshi na serikali ya Iran.
Makubaliano ya usitishaji vita yalitangazwa saa chache jana, baada ya Iran kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya kambi za jeshi la Marekani huko Qatar na Iraq.