Ulaya, Zelensky kuongea na Trump kabla ya mkutano wa Alaska
13 Agosti 2025Viongozi hao wananuia kumshawishi Trump kuheshimu maslahi ya Kyiv, atakapokutana na Rais Vladimir Putin siku ya Ijumaa huko Alaska kujadili vita vya nchini Ukraine.
Zelensky anakwenda mjini Berlin kuungana na Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani atakayeongoza mazungumzo hayo, duru za serikali ya Ujerumani zimeliambia shirika la habari la AFP.
Merz aidha amewaalika wakuu wa mataifa ya Ufaransa, Uingereza na wengine wa Ulaya pamoja na wakuu wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya NATO, kushiriki mazungumzo hayo.
Watazungumza na Rais Trump na Makamu wake JD Vance, kwenye duru ya pili ya mazungumzo hayo.
Mazungumzo hayo ya Ijumaa yamepangwa kufanyika bila ya Zelensky, hatua inayoibua wasiwasi kwamba huenda Ukraine ikalazimishwa kuingia kwenye makubaliano magumu, ikiwa ni pamoja na kuachilia ardhi yake, huku Ulaya ikisisitiza haki ya Ukraine ya kuchagua mustakabali wake.