Ulaya yazipongeza Armenia na Azerbaijan kwa mkataba wa amani
14 Machi 2025Mataifa hayo mawili ambayo yamepigana vita mara mbili vya kudhibiti eneo la Karabakh lenye idadi kubwa ya Waarmenia, yamesema walimaliza jana mazungumzo ya makubaliano hayo.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, amezipongeza pande zote mbili kwa kujitolea kwao na kuongeza kuwa tangazo hilo linawakilisha hatua madhubuti kuelekea amani na usalama wa kudumu katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Antonio Costa amewapongeza viongozi wa mataifa hayo mawili kwa makubaliano hayo.
Mara kwa mara, Armenia na Azerbaijan zimekuwa zikisema kuwa makubaliano ya kina ya amani ya kuumaliza mzozo wao wa muda mrefu yanaweza kufikiwa, lakini mazungumzo ya awali yalishindwa kufikia makubaliano juu ya rasimu ya makubaliano.