Ulaya yatoa wito kwa Israel kuondoa vikwazo vya misaada Gaza
24 Aprili 2025Mataifa ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza yameitolea mwito Israel kuondoa vikwazo vyake na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza. Vikwazo hivyo vimekuwepo kwa zaidi ya siku 50.
Mataifa hayo matatu kwenye taarifa yao ya pamoja yameonya kuhusu mzozo huo wa kibinadamu unaozidi kuwa mbaya zaidi yakisema raia wa Palestina ikiwemo watoto milioni 1 wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa,magonjwa na vifo.
Soma zaidi:Rais Mahmoud Abbas awataka Hamas waachie mamlaka ya Ukanda wa Gaza
Taarifa hiyo imeongeza kwamba misaada ya kibinadamu kamwe haipaswi kutumika kama kama chombo cha kisiasa na Israel iliyo chini ya sheria ya kimataifa inalazimika kuruhusu upitishaji wa misaada bila vikwazo.
Kulingana na utafiti wa hivi karibuni, mashirika ya misaada 43 ya kimataifa na yale ndani ya Palestina yanayofanya kazi huko Gaza yamelazimika kusimamisha au kupunguza kwa kiasi kikubwa shughuli zao tangu mashambulizi mapya ya Israel yaliyoanza Machi 18.