Ulaya yalaani vikali mashambulizi ya Urusi Ukraine
28 Agosti 2025Haya yanafanyika wakati ambapo Urusi imesema bado ina nia ya kufanya mazungumzo ya kusitisha vita vya Ukraine.
Baada ya mashambulizi hayo ya Urusi mjini Kyiv, mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amezungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa, mashambulizi hayo ni ushahidi tosha kwamba Kremlin haitoacha kuwashambulia raia, wanaume, wanawake na watoto na hata majengo ya umoja huo wa Ulaya.
Von der Leyen amesema amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump baada ya mashambulizi hayo na amesema kuwa Putin ni sharti afanye mazungumzo ya amani.
Urusi kuwekewa vikwazo zaidi
Mkuu huyo wa Umoja wa Ulaya vile vile ameapa kuiwekea Urusi shinikizo kubwa.
"Hivi karibuni tutakuja na awamu ya 19 ya vikwazo vikali. Na wakati huo huo, tunaendeleza kazi tunayofanya na raslimali za Urusi tulizozifungia ili kuchangia katika kuilinda Ukraine na ujenzi wake mpya. Na bila shaka, tutahakikisha usaidizi mkubwa kwa Ukraine, jirani yetu, mshirika, rafiki na mwanachama wa baadae," alisema Von der Leyen.
Nchi za Umoja wa Ulaya kwa sasa zinatumia riba inayopatikana kutokana na raslimali za Urusi kusaidia kuihami Ukraine na kufadhili ujenzi wake baada ya vita kufikia mwisho.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameyalaani mashambulizi hayo yaliyowalenga raia mjini Kyiv akisema hii sasa inaonesha picha kamili ya Urusi na vile vile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa amani itakayopelekea uhuru wa Ukraine na kuheshimiwa kwa mipaka yake.
Mkuu wa sera za kigeni za Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema hatua ya Urusi kuyashambulia majengo ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya ndiyo sababu kuu iliyowapelekea kumuita mjumbe wa Urusi, akisema katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba hakuna ujumbe wa kidiplomasia unaostahili kulengwa na mashambulizi.
Urusi bado inataka mazungumzo ya amani
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza ameungana na viongozi wa Umoja wa Ulaya kulaani shambulizi la Urusi huko Kyiv akisema Rais Vladimir Putin anahujumu juhudi za amani.
Haya yanafanyika wakati ambapo Kremlin imesema bado ina nia ya kufanya mazungumzo ya amani kuhusu vita vya Ukraine licha ya mashambulizi hayo yaliyofanywa mjini Kyiv.
Alipoulizwa iwapo kauli hiyo inakinzana na kile wanachokifanya katika uwanja wa mapambano, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema pande zote bado zinaendelea kushambuliana.
Vyanzo: DPAE/Reuters/AFP