Ulaya na Iran kuendeleza mazungumzo ya nyuklia
22 Agosti 2025Wanadiplomasia wa Iran wanatarajiwa kukutana na wenzao wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Tehran, wakati mataifa hayo yakizingatia kurejesha vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema mazungumzo hayo yataendelea Jumanne katika ngazi ya manaibu mawaziri wa mambo ya kigeni, akibainisha kuwa tangazo hilo limetolewa baada ya mazungumzo ya simu na wanadiplomasia wa mataifa hayo Ijumaa.
Waziri wa masuala ya kigeni wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, amethibitisha taarifa hizo kupitia mtandao wa X, akisema: "Tumekuwa na mazungumzo muhimu ya simu na wenzangu David Lammy wa Uingereza, Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani na Kaja Kallas, na mwenzetu wa Iran, kuhusu mpango wa nyuklia na vikwazo ambavyo tunapanga kuvianzisha upya.”
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani nayo imethibitisha makubaliano hayo, ikisisitiza kuwa bado inatumia njia ya diplomasia, lakini muda unazidi kuyoyoma na Iran inahitaji kushiriki kikamilifu.
Tehran inakabiliwa na muda wa mwisho wa Agosti 31 uliowekwa na mataifa hayo kufikia "makubaliano ya kuridhisha” kuhusu mpango wake wa nyuklia. Mazungumzo haya yanafuatia mapigano ya siku 12 kati ya Iran na Israel mwezi Juni, ambayo yalishuhudia Marekani ikishambulia baadhi ya vituo vya nyuklia vya Tehran baada ya kushindikana kwa makubaliano mapema mwaka huu. Iran na mataifa ya E3 wakutana Istanbul kuhusu mpango wa Nyuklia
Iran ilisitisha mazungumzo na Marekani kuhusu kufufua mkataba wa nyuklia, na tangu wakati huo wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) wameshindwa kufikia vituo vya nyuklia vya Iran, licha ya mkuu wa shirika hilo, Rafael Grossi, kusisitiza kuwa ukaguzi unabaki kuwa jambo muhimu.
Mataifa hayo matatu ya Ulaya yametishia kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran chini ya "mfumo wa masharti ya awali moja kwa moja” iwapo Tehran haitarejea kwenye meza ya mazungumzo. Mataifa hayo, pamoja na Marekani, yanasema mpango wa nyuklia wa Iran unatumika kuendeleza silaha za kinyuklia, madai ambayo Tehran imeendelea kukanusha.