Ulaya inajiandaa kuirejeshea Iran vikwazo vya UN
29 Agosti 2025Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo kabla ya mkutano wa Ulinzi wa Umoja huo mjini Copenhagen Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema kwamba katika siku 30 zijazo zitakuwa muhimu kwa mazunguzmo ya kupata suluhu katika mpango wa nyuklia wa Iran akiitaja kuwa ni fursa kwa mchakato wa kidiplomasia.
"Hakika, hizi siku 30 tunapaswa kuzitumia kikamilifu katika kupata suluhu ya kweli, ya kidiplomasia na jinsi tuitavyoweza kusonga mbele."
Alisema wasiwasi walionao kwa Iran ni kuhusu mpango wake wa nyuklia katika kutengeneza makombora na uhusiano wake na Urusi ambao unazidi kukua siku hadi siku.
"Wasiwasi wetu uwazi, hasa linapokuja suala la makombora yao. Bila kusahau msaada wao kwa Urusi."
Ujerumani, Ufaransa na Uingereza hapo jana Alhamisi zilitangaza utaratibu ambao unaweza kuirejeshea vikwazo vya Umoja wa Mataifa Iran katika muda wa siku 30 kutokana na kushindwa kwake kutekeleza ahadi zake kuhusu mpango wake wa nyuklia iliyoridhia takriban muongo mmoja uliopita.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot, amesema "Uchokozi wa nyuklia wa Iran haupaswi kwenda mbali zaidi.”
Hayo yamejiri baada ya wiki kadhaa za onyo kuhusu madai ya Iran kukiuka makubaliano ya mwaka 2015 na mataifa yenye nguvu duniani ya kuzuia mpango wake wa nyuklia. Vikwazo hivyo vilisitishwa chini ya makubaliano hayo.
Iran yaionya Ulaya dhidi ya hatua hiyo ya vikwazo
Kufuatia uamuzi huo Iran imeonya kwamba itatoa "majibu yanayofaa” dhidi ya hatua hiyo, ambayo inahatarisha kumaliza jitihada za muda mrefu zaidi za kidiplomasia kwa suluhu ya amani ya mgogoro wa nyuklia wa Iran. Lakini Umoja wa Mataifa nao umesema siku 30 zijazo ni "fursa” kwa kufikia makubaliano mapya yenye tija.
China ambaye ni mshirika wa Iran imeukosoa uamuzi huo wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, ikisema hatua hiyo "sio ya kujenga” na inaweza kudhoofisha juhudi za kidiplomasia ambazo zimeafikiwa hadi sasa.
Urusi nayo ambayo imekuwa na mahusiano ya karibu ya kijeshi na kiuchumi na Iran kwa zaidi ya muongo mmoja sasa imeonya kuwa kurejeshwa kwa vikwazo kunaweza kuleta "matokeo yasiyoweza kurekebishwa” na kusisitiza kuwa mataifa ya Ulaya yanahatarisha juhudi za kusaka suluhu ya amani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Ikumbukwe kuwa Washington na Tehran zilijaribu kurejea kwenye makubaliano mapya ya nyuklia mapema mwaka huu, lakini mazungumzo hayo yaliingia doa baada ya Israel na Marekani kushambulia maeneo ya kijeshi na nyuklia ya Iran mnamo mwezi Juni.