Ujerumani yaitisha mkutano wa video kuhusu Ukraine
11 Agosti 2025Kabla ya mkutano wa kilele wa huko Alaska siku ya Ijumaa, Rais wa Marekani Donald Trumpalipendekeza kuwa makubaliano ya amani yanaweza kujumuisha "kubadilishana baadhi ya maeneo." Lakini viongozi wa Ulaya hawajaona dalili yoyote kwamba Urusi iko tayari kutoa fursa ya hatua hiyo. Hadi wakati huu si Ulaya wala Ukraine ambayoimealikwa katika mkutano huo.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wapo katika hatua za kufanya mkutano wa dharura Jumatathu hii kwa lengo la kujadili mkutano huo kati ya marais Putin na Trump, huku Ulaya ikihofia makubaliano yoyote bila ushiriki wa Ukraine yanaweza kuwalazimisha kuridhia masharti yasiyokubalika.
Mashaka ya Ukraine kutotendewa haki
Wazo la mkutano kati ya Marekani na Urusi bila Rais Volodymyr Zelenskyy limezua hofu kwamba makubaliano hayo yanaweza kuhitaji Ukraine kukubali kupoteza maeneo makubwa ya ardhi jambo ambalo Umoja wa Ulaya unalipinga vikali.
Mwenyewe Zelenskyy ameonesha faraja kuwa na faraja ya uungwaji mkono na washirika wa Ulaya "Vita lazima vikome haraka iwezekanavyo kwa amani ya haki. Amani ya haki inahitajika. Kuna uungwaji mkono wazi kwa kanuni kwamba kila jambo linalohusu Ukraine lazima liamuliwe kwa ushiriki wa Ukraine. Kama inavyopaswa kuwa kwa kila taifa huru. Kila mtu lazima aheshimiwe. Nawashukuru wote wanaoshiriki katika msimamo huu pamoja na Ukraine."
Ujerumani yaitisha mkutano wa dharura kuhusu Ukraine
Na taarifa za hivi karibuni zinasema Ujerumani inaitisha mkutano wa dharura kwa njia ya mtandao siku ya Jumatano wa viongozi wa Ulaya kujadili mbinu za kuiwekea Urusi shinikizo ili kumaliza vita vya Ukraine, kabla ya mazungumzo ya Ulaya na Rais wa Marekani Donald Trump. Serikali ya mjini Berlin imetihibita kwa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz anapanga kufanya mashauriano siku hiyo na Rais wa Marekani Donald Trump, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, na viongozi wa Ulaya kuhusu vita vya Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy pamoja na maafisa wa Umoja wa Ulaya na NATO wanatarajiwa kushiriki mkutano huo pamoja na viongozi wa Ujerumani, Finland, Ufaransa, Uingereza, Italia na Poland. Trump amesema kuwa pande zinazohusika na vita ziko karibu kufikia makubaliano ya amani.
Na duru nyingine zinaeleza kuwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy leo hii amefanya mazungumzo marefu na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wakijadili vikwazo dhidi ya mafuta ya Urusi na kuafikiana kukutana ana kwa ana mwezi Septemba wakati wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa. Mazungumzo hayo yalizingatia pia ushirikiano wa kidiplomasia na hali ya vita, huku Zelenskyy akitambua nafasi ya India kama taifa lenye ushawishi mkubwa katika juhudi za kutafuta amani.
.