Ulaya yasalimu amri makubaliano ya biashara na Marekani
29 Julai 2025Katika kile kinachoonekana kuwa pigo kwa ndoto za Umoja wa Ulaya kujidhihirisha kama nguvu ya kiuchumi ya kujitegemea, makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen yameibua hisia mseto barani Ulaya. Makubaliano hayo yanayoanzisha ushuru wa asilimia 15 kwa bidhaa nyingi za Ulaya yanatajwa kama hatua ya kuzuia mzozo mkubwa zaidi wa kibiashara — lakini yameonekana pia kama ushahidi wa kushindwa kwa Ulaya kulinda maslahi yake kikamilifu.
Kwa mujibu wa wachambuzi, makubaliano haya ni aina ya maelewano ya maumivu ambayo yameepusha mdororo wa kiuchumi wa moja kwa moja, lakini yanatarajiwa kulifanya bara la Ulaya kudumaa kiuchumi. Benki Kuu ya Ulaya ilikuwa tayari imeonya kuwa hata viwango vya chini vya ushuru vingepunguza ukuaji wa uchumi kwa asilimia 0.5 hadi 0.9 mwaka huu, ukilinganisha na zaidi ya asilimia 1 iwapo hakungekuwa na mvutano wa kibiashara. Wengi wanasema makubaliano haya yameegemea upande mmoja — na ni ushindi kwa sera za kiuchumi za Trump.
Katika hatua ya kushangaza, Umoja wa Ulaya umejitwika mzigo wa kuwekeza dola bilioni 600 katika uchumi wa Marekani sambamba na kununua bidhaa za nishati kutoka Marekani zenye thamani ya dola bilioni 750. Mwelekeo huu umeibua wasiwasi mkubwa kuhusu uhamishaji wa uwekezaji kutoka Ulaya kwenda Marekani, na kupotea kwa uhuru wa kiuchumi wa bara hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alitoa onyo kali akisema: "Mwelekeo huu utasababisha kudhoofika zaidi kwa viwanda vya Ulaya, uhamishaji wa uwekezaji kuelekea Marekani, na bila shaka, hili litakuwa pigo kubwa — hasa katika bei za nishati, viwanda vya Ulaya, na sekta ya kilimo.”
Makubaliano bora zaidi katika mazingira magumu
Mjumbe mkuu wa mazungumzo wa Umoja wa Ulaya, Maros Sefcovic, ametetea makubaliano hayo akisema ni bora kuliko vita vya ushuru. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussels, Sefcovic alisema: "Nina uhakika wa asilimia 100 kwamba makubaliano haya ni bora kuliko vita vya kibiashara," huku akionya kuwa ushuru wa asilimia 30 ambao Trump alitishia ungeweza kuharibu kabisa biashara kati ya pande hizi mbili. Aliongeza kuwa ujumbe kutoka kwa wafanyabiashara barani Ulaya ulikuwa wazi: epukeni mvutano, tafuteni suluhu.
Hata hivyo, makubaliano hayo yameibua upinzani mkali. Waziri Mkuu wa Ufaransa, François Bayrou, ameandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa "ni siku ya giza pale ambapo muungano wa watu huru unakubali kujisalimisha." Kauli hiyo inaakisi msimamo wa Rais Emmanuel Macron ambaye awali alikuwa ameisihi Tume ya Ulaya kuchukua hatua thabiti kulinda maslahi ya bara hilo.
Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán, amezua mjadala mkali kwa kauli zake kuhusu makubaliano hayo, akiyaita ya upande mmoja na yenye udhaifu mkubwa kwa bara la Ulaya. "Kilicho wazi kwangu ni kwamba huu siyo mkataba uliofikiwa kati ya Donald Trump na Ursula von der Leyen, bali ni kama Trump alimla Ursula kwa kifungua kinywa,” alisema kwa kejeli.
Orbán pia alilinganisha makubaliano hayo na yale kati ya Marekani na Uingereza, akisema mkataba wa Uingereza ulikuwa bora zaidi. Alitilia shaka uwezo wa Ulaya kutekeleza makubaliano hayo, akihoji: "Nani atatoa mabilioni ya euro yanayopaswa kuwekezwa Marekani au kununua silaha? Tume ya Ulaya haina jeshi wala mitaji hiyo.”
Ujerumani: Heri nusu shari kuliko shari kamili
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Katherina Reiche, amekiri kuwa ushuru wa asilimia 15 ni changamoto kubwa kwa wauzaji wa bidhaa za nje wa Ujerumani, lakini amesema makubaliano hayo yanatoa uhakika wa kibiashara. Ametoa wito wa kuweka wazi kwa haraka masharti ya utekelezaji na kuhakikisha kuwa sekta muhimu kama magari, dawa, kilimo na anga zinapewa kipaumbele.
Italia, ambayo ni miongoni mwa nchi zinazonufaika zaidi na soko la Marekani, imechukua msimamo wa tahadhari. Waziri Mkuu Giorgia Meloni amesema kuwa "ni jambo jema kwamba kuna makubaliano,” lakini akasisitiza haja ya kuyachambua kwa kina kabla ya kutoa hukumu kamili. Italia ina ziada ya kibiashara ya zaidi ya euro bilioni 40 na Marekani, na serikali yake imetoa wito kwa EU kuanzisha msaada kwa sekta zitakazoathirika zaidi na ushuru huo mpya.
Kwa jumla, wachambuzi wanasema kuwa makubaliano haya hayajatatua kiini cha tatizo: utegemezi mkubwa wa Ulaya kwa soko la Marekani na ukosefu wa usawa katika sekta za kidijitali, huduma za kifedha, na usalama wa biashara ya kimataifa. Mashirika kama BGA la Ujerumani yameuita mkataba huu "tishio la kiuhai" na yanatoa wito kwa EU kuamka kutoka usingizi wa utegemezi na kujiandaa kimkakati kwa mustakabali mpya wa kiuchumi duniani.