Ukraine yataka ufafanuzi kutoka Marekani kuhusu silaha
3 Julai 2025Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky amesema nchi yake na Marekani zinaendelea na mazungumzo kuhusu taarifa hiyo ya kusimamishwa kwa shehena ya msaada wa silaha za Marekani kupelekwa nchini Ukraine.
Wizara ya Ulinzi mjini Kiev, imesema haijapokea taarifa rasmi kutoka Marekani kuhusu kusimamishwa au kuwepo na mabadiliko yoyote katika mipango ya upokeaji msaada wa kijeshi uliokubaliwa kati ya pande mbili hizo. Wizara hiyo imesema imeomba kufanyike mazungumzo ya simu na wenzao wa Marekani ili kupata ufafanuzi.
Kwa upande wake Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine imemuita naibu balozi wa Marekani mjini Kiev, John Ginkel, kujadili suala hilo la kufungiwa kupokea silaha muhimu, ambazo ziliidhinishwa wakati wa utawala wa rais wa zamani Joe Biden.
Uamuzi wa Rais Trump wa kusimamisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine umewagawa wabunge wa Marekani, baadhi yao wameonyesha wasiwasi mkubwa. Mbunge Debbie Wasserman Schultzn, ameikosoa vikali hatua ya Trump, akiashiria kuwa fedha za silaha hizo tayari zilikuwa zimeidhinishwa na Bunge na kwamba kuzizuia ni hatua inayokiuka sheria za nchi.
Kufikia sasa, hakuna uthibitisho rasmi kuhusu muda wa kuanza hatua hiyo ya kusimamisha kuipa Ukraine silaha. Hata hivyo, mijadala inayoendelea katika Bunge la Marekani na taarifa kutoka kwa wajumbe zinaonyesha kuwa suala hilo huenda likawa mada ya makabiliano ya kisiasa mjini Washington.
Wakati huo huo Ukraine na Urusi zinaendelea kushambuliana. Watu wawili wameuawa katika shambulizi la Urusi kwenye mji wa kati wa Ukraine wa Poltava. Watu 11 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa gavana wa eneo hilo Volodymyr Kohut , miundombinu ya kiraia pia imeharibiwa katika shambulio hilo.
Na kwa upande wa Urusi vifusi vya ndege isiyo na rubani ya Ukraine vimesababisha kifo cha bibi mmoja mkongwe mwenye umri wa miaka 70 katika eneo la Lipetsk, kusini mashariki mwa jiji la Moscow. Watu wawili wamejeruhiwa.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema usiku wa kuamkia leo Alhamisi imeziharibu droni 69 za Ukraine, nyingi katika eneo la Belgorod linalopakana na Ukraine.
Nalo Jeshi la anga la Ukraine, wakati huo huo, limesema lilidungua droni 40 kati ya 52 za Urusi zilizorushwa usiku wa kuamkia leo.
Vyanzo: DPA/RTRE/AFP