Ukraine yasema Urusi imefanya mashambulizi 39 ya droni
11 Aprili 2025Kutokana na mashambulizi ya Urusi, jeshi la anga nchini Ukraine limechapisha taarifa kwenye mtandao wa X, inayosema kuwa limefanikiwa kuzidungua droni 24 na kuzizuia nyingine 13 ambazo zilipoteza muelekeo na kushindwa kuyafikia maeneo yaliyonuiwa kushambuliwa. Hayo yamewezekana kwa sababu ya jeshi la Ukraine kuwa na uwezo wa kutumia hatua za kielektroniki za kivita katika kuyakabili mashambulizi.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi yailaumu Ukraine kwa kushambulia miundombinu yake ya nishati
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imeilaumu Ukraine kwa kushambulia miundombinu ya nishati ya Urusi mara tano katika muda wa saa 24 zilizopita licha ya juhudi zinazofanywa na Marekani za kufikiwa makubaliano ya kusitisha mashambulizi yanayolenga miundombinu ya nishati kati ya pande hizo mbili.
Maafisa wa US na Russia wakutana Saudi Arabia kujadili usitishaji vita Ukraine
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema katika taarifa yake kwamba Ukraine imeshambulia vituo vya nishati katika mikoa ya Kursk na Bryansk ndani ya Urusi na pia kwenye mikoa ya Ukraine ya Luhansk na Zaporizhzhia inayodhibitiwa na Urusi.
Wakati hayo yakiendelea Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema nchi yake inapanga kuipa Ukraine rada za kufanya uchunguzi wa ardhini zaidi ya 1,100 na mifumo ya ziada ya makombora ya ulinzi wa anga aina ya IRIS-T.
Waziri Pistorius amesema hii ni sehemu ya mipango ya muda mfupi na vilevile mipango ya muda mrefu ya kuiunga mkono Ukraine katika mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius ameyaeleza haya katika mkutano wa kimataifa wa kuratibu misaada zaidi ya kijeshi kwa Ukraine uliofanyika kwenye makao makuu ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO huko mjini Brussels, Ubelgiji.
Usiku wa kuamkia kwenye mkutano huo, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov, alisema suala muhimu kabisa ni kuimarisha ulinzi wa anga ya nchi yake.
Uingereza yatangaza kuongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine
Uingereza nayo imetangaza kuongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine, katika hatua za nchi za Magharibi za kuiunga mkono nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.
Mbali na ahadi za kuisaidia Ukraine kwa muda mrefu, nchi hiyo itapokea mifumo minne zaidi ya ya makombora ya ulinzi wa anga aina ya IRIS-T, makombora 300 ya kuongozwa na rada 100 za ufuatiliaji ardhini mnamo mwaka huu.