Ukraine yasema Urusi imefanya mashambulizi 39 ya droni
11 Aprili 2025Matangazo
Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi imefanya mashambulizi 39 ya droni na moja la kombora la msafara marefu katika kipindi cha siku moja iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa X, jeshi la anga limezitungua droni 24 na nyingine 13 hazikuyafikia maeneo yaliyonuiwa kushambuliwa, kutokana na uwezekano wa hatua za kielektroniki za kivita kuyakabili mashambulizi.
Wakati haya yakiarifiwa utawala wa Kremlin umesema leo kwamba mjumbe maalumu wa rais wa Marekani Donald Trump kwa mzozo wa Ukraine, Steve Witkoff, anafanya ziara mjini Moscow.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amethibitisha ziara hiyo ya Witkoff na kusema Urusi itatoa taarifa kama mjumbe huyo atakutana na rais wa Urusi Vladimir Putin.