Ukraine yasema inao uwezo wa kuendelea kupambana na Urusi
4 Machi 2025Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal amesema nchi hiyo ingali inao uwezo wa kuvipatia vikosi vyake zana na mahitaji yote muhimu kuendelea kupigana na Urusi kwenye eneo la mstari wa mbele wa vita.
Alikuwa akizungumza saa chache baada ya Ikulu ya White House kutangaza kuwa Rais Donald Trump ameamuru kusitishwa kwa muda msaada wote wa kijeshi kwa Ukraine.
Shmyhal amesema lakini utawala mjini Kyiv ungependelea bado kuwa na mahusiano ya karibu na Marekani akiitaja nchi hiyo kuwa mshirika muhimu kwa Ukraine.
"Tutaendelea kufanya kazi na Marekani, na bunge la Marekani na utawala wa Trump kwa kutumia njia za kidiplomasia zilizopo na (tena) kwa hali ya utulivu, ili Ukraine na Marekani ziendelea kupigania amani ya haki, ya kudumu na madhubuti kwa Ukraine na bara la Ulaya." amesema kiongozi huyo wa Ukraine.
Mbali ya mahusiano, Waziri Mkuu Shmyhal amesema Ukraine inatafuta uhakika na dhamana ya ulinzi kutoka kwa Marekani na washirika wa magharibi akilitaja hilo kuwa "kitu muhimu sana" kwa Ukraine pamoja na Ulaya. Ameongeza pia Ukraine iko tayari wakati wowote kutia saini mkataba wa madini adimu na Marekani ambao umekuwa ukishinikizwa na Trump.
Zelensky ajizuia kuzungumzia uamuzi wa Marekani, Urusi yaupongeza
Kwa upande wake Rais Volodymyr Zelenskiy ambaye msuguano wake na Rais Trump unatajwa kuwa sababu ya Marekani kuzuia msaada wa kijeshi wa Ukraine, amechagua kukaa kimya tangu tangazo la kusitishwa misaada lilipotolewa usiku wa kuamkia leo.
Kiongozi huyo badala yake alifanya mazungumzo na mwanasiasa anayetarajiwa kuwa kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz na baadaye akatumia mitandao ya kijamii kuishukuru Ujerumani kwa mchango mkubwa wa kijeshi na kifedha inaoutoa kwa Ukraine.
Nchini Urusi taarifa za kusitishwa msaada wa kijeshi kwa Ukraine umesifiwa na ikulu ya Kremlin. Msemaji wa Rais Vladimir Putin, Dmitry Peskov amesema uamuzi huo wa Trump ni suluhisho litakaloulazimisha utawala mjini Kyiv kuingia kwenye mchakato wa kusaka amani.
Amesema iwapo Marekani itatimiza kwa vitendo usitishaji wa kupeleka silaha Ukraine itakuwa imetoa mchango ulio bora sana kwenye kusaka amani.
Washirika wa Ulaya waingia kiwewe na uamuzi wa Marekani
Kwa muda muda mrefu hata kabla ya kuanza kwa vita vya sasa, Ukraine imekuwa ikitegemea msaada mkubwa wa kijeshi kutoka Marekani.
Tangazo la kusitishwa kwake limezusha hamkani miongoni mwa washirika wa Marekani barani Ulaya ambao wanahisi Washington imechagua kusukuma ajenda yake ya kufikia makubaliano ya amani na Urusi bila kujali taathira kwa upande wa Ukraine.
Ufaransa imekosoa uamuzi huo wa Marekani ikisema kupitia waziri wake anayeshughulikia masuala ya Ulaya , Benjamin Haddad, kwamba Washington inafanya "amani iwe mbali kupatikana" kwa sababu imechagua kuimarisha nafasi ya Urusi aloitaja kuwa "mchokozi".
Uingereza yenyewe imechagua kujiepusha kuzungumzia suala hilo na badala yake imesema Waziri Mkuu Keir Starmer alizungumza na Trump jana usiku kwa dhamira ya kuiwaka karibu Marekani na washirika wake wa Ulaya.
Serikali ya Poland imesema Marekani imechukua uamuzi huo bila kuwashirikisha mataifa washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kwamba athari ya hatua hiyo tayari zimeanza kuonekana kwa kuzuiwa usafirishwaji silaha kwenda Ukraine kutokea mabohari yaliyoko Poland.