Ukraine yaunga mkono usitishwaji mapigano wa siku 30
12 Machi 2025Taarifa ya pamoja ya Kyiv na maafisa wa Marekani baada ya mkutano uliofanyika mjini Jeddah, Saudi Arabia, ilisema Ukraine inaafikiana na pendekezo hilo.
Rais Volodymyr Zelensky amesema Marekani watajaribu kuishawishi Urusi kukubaliana na pendekezo hilo katika matamshi yake ya jana jioni na kulingana na taarifa hiyo ya pamoja, Marekani itawasiliana na Urusi ambayo pia ni muhimu kuelekea mustakabali wa amani baina ya mataifa hayo mawili.
Soma pia:Ukraine na Marekani wajadili mpango wa kusitisha vita
Msaidizi wa ngazi wa juu wa Zelensky amesema walijadiliana pia na maafisa wa Marekani juu ya dhamana za kiusalama kwa Ukraine, ingawa hakutoa maelezo zaidi.
Marekani yaahidi kurejesha ushirikiano na Ukraine
Marekani aidha imesema itarejesha utaratibu wa kuipatia Ukraine taarifa za kiintelijensia na msaada wa kiulinzi, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akisema macho sasa yanaelekezwa kwa Urusi ikiwa itaamua kukubaliana na pendekezo hilo ama la.
Marekani na Ukraine aidha wamekubalina kusaini mara moja makubaliano ya kuendeleza rasilimali muhimu ya madini ya Ukraine.
Mengi yamejitokeza baada ya taarifa hizi kutoka Jeddah. Rais Donald Trump wa Marekani amesema sasa anapanga kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin moja kwa moja baada ya hatua hii ya Kyiv. Akasema, Urusi inalazimika kukubaliana kwanza na usitishwaji wa mapigano na kuongeza kuwa ana imani kwamba Putin atakubaliana nayo.
Kwa ujumla, Trump tayari ameonyesha matumaini makubwa ya kuvimaliza vita baada ya makubaliano haya ya Jeddah.
Mshauri wake kwenye masuala ya Usalama wa Taifa Mike Waltz kwa upande wake amesema, swali lililopo sasa si "kama" ila "ni kwa namna gani" vita hivyo vitamalizwa.
Soma pia:Ukraine itarajie nini kutokana na mazungumzo, Saudi Arabia?
Ulaya yakaribisha makubaliano licha ya kutengwa
Ulaya ambayo hata hivyo haikuhusishwa kwenye meza ya majadiliano ya Jeddah imeyakaribisha kwa mikono miwili tmakubaliano hayo ya kusitisha vita kwa muda. Wa kwanza alikuwa ni Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen, aliyeandika kwenye mtandao wa X akisema hii ni hatua nzuri kuelekea kupatikana amani ya kudumu nchini Ukraine. Pamoja naye, alikuwa ni Rais wa Baraza la Ulaya Antionio Costa. Wakamalizia kwa kusema, mpira sasa uko upande wa Urusi.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, aliyaita makubaliano hayo kuwa ni hatua muhimu kuelekea amani na kusema, Ulaya iko tayari kusaidia kufikiwa kwa amani ya kudumu.
soma pia:Viongozi wa Ulaya wanakutana London kujadili migogoro
Ujerumani imesema kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje Annalena Baerbock kwamba hatua hii imebadilisha pakubwa hali ya mambo na kuongeza kuwa wako tayari kuwasaidia watu wa Ukraine kufanikisha mchakato wa amani.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia ameikaribisha hatua hiyo na hakutofautiana na wakuu wa Umoja wa Ulaya kwa kusema ni wazi mpira sasa uko kwa Urusi.
Kutokea London, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer pia aliyaunga mkono makubaliano hayo akiyataja kama mafanikio makubwa. Aliandika kupitia mtandao wa X kwamba wako tayari kuvimaliza vita nchini Ukraine. Siku ya Jumamosi, Starmer atazungumza kwa simu na viongozi waliopo kwenye kile kinachotajwa kama "coalition of the willing" kujadili juhudi za amani nchini Ukraine.
Soma pia