Ukraine yaripoti visa vya ukiukaji wa usitishaji vita
21 Aprili 2025Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema mapema leo kwamba vikosi vya Ukraine vimeripoti matukio 2,935 ya ukiukaji wa ahadi ya usitishaji wa mapigano uliotangazwa na Urusi.
Zelensky amesema aina ya hatua za Ukraine zitaendelea kutegemea hatua zinazochukuliwa na Urusi. Rais huyo pia amesema watajibu ukimya kwa ukimya na mashambulizi yao yatalenga kujilinda dhidi ya mashambili ya Urusi.
Urusi na Ukraine zimetuhumiana kwa kukiuka mkataba wa kusitisha mapigano katika kipindi cha Pasaka huku rais wa Marekani Donald Trump akitoa tangazo la kushangaza kwamba mahasimu hao wawili huenda wakafikia makubaliano wiki hii.
Usitishaji huo wa mapigano wa saa 30 kuanzia Jumamosi iliyopita, uliotangazwa na rais wa Urusi Vladimir Putin, ulinuiwa kuanzisha likizo ya Pasaka lakini rais Zelensky akasema Urusi ilikuwa imefanya mamia ya mashambulizi katika uwanja wa mapambano.